MCHAKATO WA WATU KUACHANA HUANZA HIVI, KUWA MAKINI

NA RAMADHANI MASENGA


 

WATU wengi huamini tukio la kuachana ni la siku moja ila kitaalamu tunaamini siku ya kutengana si siku watu walipoamua kuachana.

Kuachana ni mchakato unaotokana na matendo ya wahusika kwa muda mrefu. Iko hivi, namna unavyomkera na kumuumiza ndivyo unavyoua nguvu yake ya upendo kwako na kuamsha hisia hasi dhidi yako kitu kinachopelekea watu kuachana.

Kama ambavyo kuna watu kutokana na mtindo wao wa maisha kila siku wanaamsha hisia zao za upendo na kujaliana ndivyo pia kuna watu kutokana na mwenendo wao huwa wanaua nguvu yao ya upendo kila siku. Kwa namna hii hawa watu wakifikia kutengana haina maana kwamba hilo ni tukio la siku moja. Kuachana kwao lilikuwa ni suala la mchakato wa muda mrefu ila kutengana kwao ndilo suala ambalo linaweza kutokea siku moja.

Wapenzi wanatakiwa kujua kitu kimoja muhimu. Matendo yao ya kujali, kuthamini na kiubunifu ndiyo yenye kujenga uimara wa mapenzi na si kukaa na kulalamika au kuanza kusubiri wao ndio waanze kutendewa matendo yanayowafurahisha tu.

Binti mmoja alikuja ofisini na kuuliza afanye nini ili mpenzi wake asiweze kumwacha! Kwa mujibu wa maelezo yake alisema huko nyuma amewahi kuwa na wapenzi kadhaa ila mbali na uzuri na urembo wake waliishia kumwacha na kujikuta mara kadhaa akiwa katika mahusiano mapya.

Baada ya kuzungumza kwa takribani saa moja na dakika kadhaa, tatizo lililokuwa likimsumbua likajiweka bayana. Urembo wake ulikuwa unamfanya awe anajifikiria zaidi yeye (self arbsobed) kuliko alivyokuwa akimfikiria mpenzi wake.

Yeye ndiye alijiona ana haki ya kusikilizwa, kufuatishwa na kufurahishwa. Na kwa sababu za kimapenzi, wanaume aliokuwa nao walijikuta wakitekeleza hili suala vizuri na kwa uhodari wa hali ya juu. Matokeo yake yeye alizidi kuvutiwa nao kwa sababu alikuwa akitendewa mambo yanayomfurahisha ila kwa kuwa yeye alikuwa akipenda kujijali yeye tu na si wenzake, alishindwa kuwapa raha na furaha stahili ndiyo maana kwao haikuwa kazi ngumu kutengana naye.

Huyu binti mwanzo alikuwa akipendwa na kujaliwa na wenzake ila kadiri siku zilivyokuwa zikisonga ule upendo uliokuwa baina yao ulizidi kukosa nguvu kutokana na aina ya tabia yake na hatimaye akajikuta akiachwa.

Unafanya nini katika mahusiano yako? Kitu gani unakifanya kwa mwenzako chenye kukupa thamani na hadhi stahili?

Kumbuka ikiwa humfanyi mwenzako akuone bora, wa thamani na hadhi si tu unamfanya asifurahie kuwa na wewe katika maisha yake ila pia unamfanya awe tayari kuishi bila wewe muda wowote. Matendo yako kwa mwenzako ndiyo yenye kuamua kiwango cha upendo cha mwenzako juu yako.

Watu hawaachani kama ajali ila husukumwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali na nyingi ni za muda mrefu.

Kila tendo lako kwa mwenzako ni ama linaenda kuongeza nguvu ya upendo ama kutia udhaifu upendo wake kwako, jukumu ni lako sasa.

Watu wengi wamekuwa wakifikiria tu juu ya siku wanayotengana wakidhani ndiyo tatizo kubwa. Hapana. Mfululizo wa makosa yako ama namna usivyomfanya mwenzako ajivunie kuwa na wewe ndiyo yenye kumjaza hamasa ya kutaka kuachana na wewe.

Mfuatano wa maudhi uliyomfanyia kwa miaka kadhaa ndiyo yanayompa ujasiri wa kuona anafaa kuishi bila wewe na ndipo mnatengana rasmi.

Mapenzi ni suala la kupeana, furaha, raha na kumbukumbu nzuri. Kama unampa kero na karaha kisha hana lolote la kujivunia toka kwako ni kwanini asipate hamasa ya kuamini bila wewe atakuwa na furaha na amani?

Usidharau kitu katika mahusiano yako. Kauli na matendo yako ni chanzo chake cha furaha ama huzuni. Kama unahisi mwenzako anakosa amani, kuwa mfariji na burudani yake.

Kuamini wewe tu ndiye mwenye hadhi na kustahili kujaliwa na kusikilizwa si tu unakosea ila pia unajipa alama mbaya sana katika nafsi yake. Alama ambayo itampa sababu ya kukuona hufai katika maisha yake.

Wapo watu waliotengana na wapenzi wao wanafurahia hali hiyo ila pia wapo watu waliotengana na wapenzi wao ila wapenzi hao mpaka sasa hali yao ya kifikra bado haiko sawa hata kidogo. Sababu ni nyepesi tu.

Yule aliyetengana na mpenzi wake na mwenzake anafurahia hali hiyo ni kwa sababu katika mahusiano yao hakuwahi kumpa mwenzake anayostahili na kwa ubora na hadhi ya hali ya juu. Ila kwa upande wa yule aliyetengana na mpenzi wake na mwenzake mpaka sasa hayuko katika hali nzuri kifikra, ni kwa sababu utengano umemfanya akose raha, furaha na burudani aliyokuwa akiipata. Ukitengana leo na mwenzako atakuwa na hali gani?

Kumjali mwenzako si tu ni kwa faida yake ila ni kwa faida yako pia kwa sababu upendo wako kwake pia unaenda kumfanya akutegemee kwa furaha yake hali inayoongeza upendo wake kwako na kujikuta akihofia kabisa kukupoteza katika maisha yake.

Instgram: ramadhani.masenga

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia (Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*