MBEYA CITY WAITAHADHARISHA YANGA KWA IHEFU FC

NA WINFRIDA MTOI

TIMU ya soka ya Mbeya City imeitahadharisha Yanga juu ya timu ya Ihefu FC, kuwa wasitarajie mteremko, kwani kikosi hicho kina wachezaji wanaopambana na ushirikiano uwanjani.

Yanga inatarajia kukutana na Ihefu, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL), katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam, itakayopigwa katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, mwishoni mwa mwezi huu.

Ihefu ilitinga hatua hiyo ya 32 bora baada ya kuitoa Mbeya City katika michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti 5-4, kutokana na sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, mchezo uliochezwa Sokoine, Desemba, mwaka jana.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Mohamed Kijuso na straika wa kikosi hicho, Eliud Ambokile, walisema Yanga wasijaribu kuidharau timu hiyo, kwani inaweza kuwatoa.

“Si timu yenye wachezaji maarufu sana, lakini wanapokuwa uwanjani wanacheza kwa kujitolea na ushirikiano kila idara, hivyo Yanga wanatakiwa kujiandaa zaidi,” alisema Kijuso.

“Ihefu nilivyoiona ni timu nzuri, lakini mpira huwa unabadilika, inawezekana wametufunga sisi na wao wakafungwa mechi ijayo, ila Yanga wasitarajie mteremko wakidhani ni timu ndogo, wachezaji wake wanajua kupambana kusaka matokeo mazuri,” alisema Ambokile.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*