Mbeya City kuhamishia mauaji Coastal Union

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo, amesema Coastal Union ijiandae kwa kichapo watakapokutana katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya City ambayo wiki iliyopita imetoka kuichapa African Lyon mabao 4-1, kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, itacheza na Coastal Union Desemba 9, mwaka huu, Mkwakwani, Tanga.

Akizungumza na BINGWA jana kwa simu kutoka Mbeya, Nsanzurwimo, alisema  mchezo ujao wanatarajia kucheza ugenini lakini  wamejipanga kuendeleza ushindi.

Alisema sababu ya kufanya vizuri wanayo kutokana na  kuimarika kwa kikosi chake pamoja na ushirikiano uliopo kati ya viongozi, benchi la ufundi, mashabiki katika kuhakikisha wanakusanya pointi kwa kila mechi.

“Kuna ushirikiano mkubwa kati ya Wanambeya wote, hali hii ikiendelea pamoja na kujituma kwa wachezaji tutaendelea kupata ushindi mzuri kwa mechi nyingi,” alisema Nsanzurwimo.

Alifafanua kuwa baada ya wadau wa Mbeya kuwa karibu na timu hiyo, morali ya wachezaji imekuwa juu tofauti na mechi za nyuma kwa sababu wana uhakika wakupata mahitaji yao yote.

Ushindi wa mabao 4-1 waliopata dhidi ya African Lyon umewaongezea ujasiri wa kuendelea kushinda michezo ijayo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Mbeya City wapo nafasi ya tano na pointi 22 baada ya kushuka dimbani mara 15, ikishinda mechi sita, sare nne na kupoteza tano.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*