googleAds

MBELGIJI SIMBA ATOA KALI

NA ZAITUNI KIBWANA


WAKATI  Simba ikishuka uwanjani leo kukipiga na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, amesema toka ameanza kufundisha soka hajawahi kuwa na kikosi bora na kipana kama cha Wekundu wa Msimbazi hao.

Simba msimu huu inaonekana kuwa na kikosi kilichosheheni wachezaji wa kiwango cha juu kutoka ndani na nje ya nchi, japo hadi sasa imepoteza pointi saba katika kipute cha Ligi Kuu Bara.

Wakiwa kama mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba wameshinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza mmoja dhidi ya Mbao FC ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza na BINGWA juzi, Mbelgiji huyo alisema tangu ameanza kazi ya kufundisha soka kuanzia mwaka 1990, hajawahi kukutana na timu yenye wachezaji wasikivu na yenye kikosi kipana kama cha Simba.

“Sijawahi kukutana na timu ambayo ina wachezaji wasikivu kama Simba, ndio maana natumia uzoefu wangu wote kuhakikisha nawasaidia kutimiza malengo yao.

“Nina imani wakiendelea hivi wanaweza kufanya vizuri katika mechi zote za ligi na hata zile za kimaraifa,” alisema.

Akizungumzia mchezo wao wa leo dhidi ya Lyon, Aussems alisema amewaandaa vijana wake kusaka alama tatu muhimu hasa baada ya kutoka suluhu dhidi ya Yanga Jumapili ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Tumejiandaa kwa ajili ya kuvuna pointi tatu, hatuidharau African Lyon lakini wasitarajie mteremko kwetu, lengo letu ni kuendelea kujiweka pazuri kwenye msimamo wa mechi za mapema ili tusipate tabu mwishoni,” alisema.

Alisema leo (jana) nyota wao waliokuwa timu ya Taifa, Taifa Stars,  inayojiandaa kuifuata Cape Verde kuvaana nayo katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019) zitakazopigwa nchini Cameroon mwakani, wanatarajia kujumuika nao.

Nyota wa Simba waliopo katika kikosi cha Stars ni Jonas Mkude, John Bocco, Aishi Manula na Shomari Kapombe.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara hadi jana, Simba iliyojikusanyia pointi 11 kutokana na mechi sita, ilikuwa ikishika nafasi ya 8 kutokana na michezo saba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*