MBELGIJI AWASHTUKIA JKT TZ

NA OSCAR ASSENGA, TANGA


KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ameshtukia mpango mzima wa JKT Tanzania kuhamisha mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, akidaiwa wapinzani wao wametaka washindwe kucheza vizuri.

Kocha huyo wa Ubelgiji alisema hayo jana muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazoezi yao ya mwisho na kupata fursa ya kuuona uwanja huo na kuweka wazi kwamba, hatarajii mchezo mzuri.

Kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime ambaye timu yake itaavana na Simba leo, aliamua kuchagua uwanja huo wa Mkwakwani kucheza mechi yao ambayo ingetakiwa kupigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kutokana na ule wa kwao wa Isamuhyo kuwa mdogo.

Maamuzi hayo yameonekana kutomfurahisha Aussems ambaye ametoa maagizo kuwa uwanja huo wa Mkwakwani umwagiwe maji ili waweze kuutumia leo Jumamosi kwenye mechi hiyo.

“Sina uhakika kama leo kutakuwa na mechi nzuri kutokana na hali ya uwanja kutokuwa nzuri, hivyo mpira hautakuwa mzuri lakini kama wataumwagia maji angalau unaweza kuwa mzuri,” alisema Aussems.

Lakini pamoja na uwanja kutokuwa mzuri, Aussems amesema kikosi chake kitahakikisha kinaondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo kwa kuwa ni muhimu sana.

Pia kocha huyo amempa kazi maalumu mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi, ili kuhakikisha anawaliza JKT Tanzania.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, kocha huyo alimwita Okwi na kuzungumza naye kwa muda mrefu na watu waliosogelea karibu wanadai kwamba alimwagiza mshambuliaji huyo afunge katika mechi hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*