Mbappe atabiriwa kumfikia De Lima

PARIS, Ufaransa

NYOTA wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Youri Djorkaeff, amesema kwamba straika wa vinara wa soka katika michuano ya Ligue 1, Paris Saint Germains, Kylian Mbappe,  kwa sasa yupo sawa na Thierry Henry, lakini akasema kuwa atamfikia Ronaldo de Lima, katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Mbappe mwenye umri wa miaka 19, tayari kwa sasa anasemekana kuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani na juzi alishika nafasi ya nne katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka  ya dunia,  Ballon d’Or, baada ya kuwa na mwaka mzuri akiwa na timu yake ya PSG na ya Taifa ya Ufaransa.

Msimu huu, straika huyo kinda ameisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia na huku tayari ameshafunga mabao 14 katika mechi 15 alizokwisha ichezea PSG.

Kufuatia mafanikio hayo, Djorkaeff, ambaye aliisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka  1998, anasema kwamba katika mawazo yake anafikiri  Mbappe  kwa sasa ni kama Henry, lakini hivi karibuni atakuwa kama kinara wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldo.

“Ana bahati ya kucheza na mastraika mahiri. Na ninavyofikiri Mbappe ni mzuri kama  Thierry Henry, kwa sababu ana kasi kama yake,” mkongwe huyo aliuambia mtandao wa  Omnisport.

“Ronaldo alikuwa akiunasa mpira akageuka, akapiga chenga kwa kasi na umahiri wa hali ya juu. Lakini Mbappe anapenda kuambaa na mpira kama alivyokuwa akifanya Thierry Henry,” aliongeza nyota huyo wa zamani.

“Ronaldo alikuwa akicheza namba tisa. Mbappe anacheza pembeni kama alivyokuwa akifanya Thierry Henry. Hivyo nadhani katika kipindi cha miaka miwili ama mitatu tutakuwa tukimfananisha Mbappe  na Ronaldo kwa sababu kwa mujibu wangu mimi,  Mbappe atakuja kucheza namba tisa,” alikwenda mbali zaidi mkongwe huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*