Maua Sama anogesha uzinduzi nywele mpya za Darling

NA MWANDISHI WETU

MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Maua Sama, amenogesha vilivyo uzinduzi wa nywele mpya za Kampuni ya Darling za rangi ya zambarau, tukio lililofanyika  mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa  King Solomon, Dar es Salaam.

Katika uzinduzi huo uliopambwa na onyesho la mavazi kutoka kwa wanamitindo wakali hapa nchini, umati uliohudhuria tukio hilo ulipewa zawadi za nywele mbalimbali za Darling kama sehemu ya kuonyesha shukurani kwao kwa kuwa karibu na bidhaa hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Mkuu wa Darling Tanzania, Manish Kumar, alisema wameona ni vema kubadili rangi ya nywele zao ili kuzidi kuwafanya wateja wao wapendeze zaidi, kwani bidhaa yao hiyo ipo katika ubora wa hali ya juu.

“Rangi ya zambarau ina mvuto wa aina yake, humfanya mwanamke kupendeza zaidi kwani nywele za Darling humfanya mtumiaji kubaini uzuri wake.

“Nywele zetu zipo katika ubora wa hali ya juu, bei yake ni rahisi na hudumu kwa muda mrefu bila kuharikiba haraka,” alisema.

Alisema mbali na nywele za rangi hiyo mpya ya zambarau, pia mifuko inayobeba bidhaa zao ipo katika rangi hiyo kutoka nyekundu iliyozoeleka.

Aliwataka wateja wao kuzichangamkia nywele hizo kwani zitawafanya kuonekana warembo zaidi.

Alisema mbali na Tanzania, bidhaa zao hizo zimesambaa katika nchi nyingi za Afrika kama Uganda, Kenya, Afrika Kusini, Zambia, Nigeria, Ghana na Msumbiji chini ya kampuni mama ya Godrej yenye maskani yake India.  

Wakizizungumzia nywele za Darling, baadhi ya wateja wa bidhaa hiyo walisema wataendelea kuzitumia, kwani ni kimbilio la wengi kwa muda mrefu kutokana na ubora wake lakini pia unafuu wa bei.

Benard Yusuph wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam ambaye  ni mfanyabiashara wa nywele hizo aliyekuwapo katika tukio hilo, alisema: “Wateja wangu wanazipenda sana nywele za Darling kwani ni laini, bei yake ni nafuu na hudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko bidhaa nyingine.”

Mbali na Maua Sama, DJ mahiri wa Clouds Media, DJ Sinyorita, alifanya mambo makubwa na kukonga nyoyo za umati uliojitokeza ukumbini hapo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*