googleAds

MATUKIO YA MICHEZO YALIYOTIKISA APRILI 2016

NA MWANDISHI WETU,

TUNAZIDI kuhesabu siku kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 ambao tunamatumaini utakuwa wa mafanikio katika sekta ya michezo. Leo BINGWA linakuletea matukio ya michezo yaliyojiri Aprili mwaka 2016:-

*TFF yashusha rungu kali

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imezikuta na hatia ya upangaji matokeo klabu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) na kuzishusha daraja mpaka Ligi Daraja la Pili (SDL) huku JKT Kanembwa ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL).

Aidha, kamati imemkuta na hatia kocha msaidizi wa Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na soka wakati magolikipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold wakifungiwa miaka 10 kutojihusisha na soka, ikiwamo kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 10 kila mmoja.

Walioepuka adhabu kali ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (Gerefa), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu Mkuu wa klabu ya JKT Kanembwa, Basil Matei.

*Ravia ndio bosi ZFA

Ravia Idarous ameshinda nafasi ya urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kama ilivyotarajiwa na wadau wengi wa soka katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Mshindi alipata kura 47 na kumbwaga mpinzani wake Salum Bausi Nassor aliyeambulia kura sita kati ya 53 zilizopigwa, huku Ali Mohammed Ali aliyewania tena nafasi ya Makamu wa Rais ofisi ya Pemba alipeta baada ya kuvuna kura 46 akimshinda Sued Hamad aliyepata kura saba.

Nafasi ya Makamu wa Rais upande wa Unguja, imechukuliwa na Mzee Zam Ali aliyepata kura 37, akiwashinda Mohammed Masoud Rashid na Ali Salum Mkweche waliopata kura 11 na tano mtawalia.

*Azam safari imewadia

Ushindi mwembamba wa mabo 2-1 ambao Azam FC waliupata dhidi ya Espérance de Tunis ya Tunisia katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam, uliwaweka njiapanda kufuzu hatua inayofuata Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mchezo huo, mabao ya Azam FC yalifungwa na Farid Mussa na Ramadhani Singano huku lile la Espérance likifungwa na Haythem Jouini.

Azam FC walishindwa kulinda ushindi wao mwembamba katika mchezo wa marudiano baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 yaliyofungwa na Saad Bguir, Jouini na Fakhreddine Ben Youssef.

*Yanga ndio basi tena 

Yanga yashindwa kuiondoa Al Ahly ya Misri na kutinga hatua ya makundi Klabu Bingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 ambapo Al Ahly walitangulia kupata bao dakika ya 10 lililofungwa na Amr Gamal, huku Ahmed Hegazy akijifunga dakika tisa baadaye.

Mchezo wa marudiano uliochezwa mjini Alexandria, Misri ulikuwa wa kuvutia ambapo wenyeji walipata bao la kuongoza dakika ya 51 lililofungwa na Hossam Ghaly kabla ya Donald Ngoma kuisawazishia Yanga dakika ya 66. Huku wengi wakidhani mchezo huo utaamuliwa kwa matuta, Abdallah Said aliipatia Al Ahly bao la ushindi dakika za mwisho.

*Mbao FC kama zali vile

Mbao FC ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya tatu Kundi C Ligi Daraja la Kwanza, imepandishwa daraja kucheza Ligi Kuu Bara na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

TFF imeitangaza Mbao FC kufuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF ya kuzishusha daraja timu nne kutoka Kundi C baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo.

Timu ambayo matokeo yake yamefutwa ni Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembwa hivyo basi Mbao FC inaungana na African Lyon na Ruvu Shooting kucheza Ligi Kuu Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*