googleAds

MATOLA AMUOTA SALAMBA

NA TIMA SIKILO


 

KOCHA Mkuu wa Lipuli, Suleiman Matola, amesema bado pengo la mshambuliaji Adam Salamba halijapata mbadala wake.

Salamba, ambaye alisajiliwa na Simba, alikuwa mshambuliaji tegemeo ndani ya kikosi hicho, ndiyo maana Matola amekiri wazi kwamba kuna pengo kwenye kikosi chake tangu aondoke.

Akizungumza na BINGWA juzi, Matola alisema Salamba alikuwa na mchango mkubwa sana kutokana na uwezo aliokuwa nao na kwamba anatafuta namna bora ya kuwasuka washambuliaji wake ili kumsahau kabisa.

“Bado tuna pengo la Salamba, kwani alikuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi chetu, tunaendelea kufanya juhudi za kuwasuka washambuliaji waliopo ili kuhakikisha wanafanya vizuri,” alisema.

Akizungumzia Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, alisema timu nyingi zimejiandaa vizuri, ndiyo maana Ligi inakuwa ngumu, lakini yeye na kikosi chake watahakikisha wanapata matokeo mazuri kila mchezo.

“Hakuna timu rahisi, ndiyo maana unaona ligi ni ngumu, lakini yote kwa yote sisi Lipuli tumejiwekea malengo ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*