MASTAA YANGA WALIOTWAA TAJI AFRIKA MASHARIKI NA KATI 1993 (4)

NA HENRY PAUL

WIKI iliyopita BINGWA Jumatatu katika toleo la pili, lilikumbusha baadhi ya wachezaji wa zamani wa Yanga waliotwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuifunga Club Sports Villa ya Uganda mabao 2-1. Mabao katika mchezo huo yalifungwa na Edibily Lunyamila na Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu).

Mchezo huo wa fainali ambao ulikuwa ni mkali na wa kusisimua kwa muda wote wa dakika 90, ulichezwa kwenye Uwanja wa Nakivubo, mjini Kampala, Uganda, Jumamosi 30, 1993.   

Ufuatao ni mwendelezo wa baadhi ya wachezaji hao ambao wanakumbukwa hadi leo hii na wapenzi wa soka nchini hususan wa klabu ya Yanga kwa kutwaa taji hilo.

11.SAID MWAMBA ‘KIZOTA’

Mshambuliaji Mwamba au Kizota kama wapenzi wa soka nchini walivyozoea kumwita, ni miongoni mwa wachezaji wa klabu ya Yanga waliosajiliwa mwaka huo wa 1993 na ndiye aliyefunga bao la kwanza katika mchezo wa fainali dhidi ya Club Sports Villa, katika dakika ya sita na bao la pili ambalo lilikuwa ni la ushindi lilifungwa na winga wa kushoto Edibily Lunyamila, dakika mbili kabla ya mapumziko.

Mpachikaji huyo wa mabao Mwamba ambaye hivi sasa ni marehemu katika michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao sita.

Mwamba kabla ya kupata umaarufu katika ulimwengu wa soka, Februari mwaka 1987 alichezea klabu ya Kurugenzi Dodoma katika michuano maalumu ya kusherehekea miaka 10 ya kuzaliwa kwa CCM ambayo ilifanyika katika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma, huku akitokea Tindo ya Tabora.

Katika michuano hiyo, Mwamba aling’ara mno na baada ya mashindano hayo kumalizika kutokana na kwamba alikuwa hajasajiliwa klabu ya Kurugenzi ya Dodoma, alirudi tena Tabora katika klabu yake ya Tindo na baadaye kuibukia katika michuano ya Taifa Cup akichezea timu ya Mkoa wa Tabora.

Mashindano hayo ya Taifa Cup ya mwaka huo wa 1987 yalifanyika kwenye Uwanja wa Kurume, Ilala, jijini Dar es Salaam na Mwamba kung’ara tena.

Hivyo mwishoni mwa mwaka 1987 baada ya Yanga kuvutiwa na uchezaji wake, ndipo walipoamua kumfuata na kumsajili kwa msimu wa 1988/1989 na kuanza rasmi kuichezea klabu hiyo kongwe yenye maskani yake makuu mtaa wa Jangwani na Twiga.

Baada ya kusajiliwa na Yanga msimu huo katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), Mwamba akicheza nafasi ya kiungo mkabaji, alianza kuonesha vitu adimu ambavyo si vya kawaida na kuanza kuwa kipenzi mkubwa wa wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga.

Baada ya kuichezea kwa takriban miaka mitatu hivi au minne kutokana na Yanga kutokuwa na wapachikaji mabao mahiri, Kizota alisogezwa mbele akawa anacheza namba tisa na 10 na akawa ni mmoja wa wapachikaji mabao tegemeo wa klabu hiyo.

Mwamba pamoja na kuichezea Yanga kwa mafanikio, pia ameichezea Posta ya Tabora, Kurugenzi ya Dodoma, timu ya Mkoa wa Dar es Salaam maarufu Mzizima United, Al-Nasor ya Oman na timu ya taifa, Taifa Stars.

12.MOHAMED HUSSEIN ‘MMACHINGA’

Mshambuliaji wa kati Hussein maarufu Mmachinga, ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga waliocheza fainali dhidi ya Club Sports Villa ya Uganda, mwaka huo wa 1993, huku akicheza safu ya mshambuliaji wa kati na timu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Jangwani na Twiga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. 

Nyota huyo alisifika kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa nao wa kupachika mabao, mashuti makali hali iliyowafanya magolikipa wa timu pinzani alizokuwa anacheza nazo kupata wakati mgumu kudaka michomo yake.

Mkongwe huyo ambaye alistaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 2001, alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka miaka ya 1980 mwishoni alipokuwa anachezea timu ya Bandari ya Mtwara.

Kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa akiuonesha nyota huyo wa kupachika mabao, mwaka 1993 klabu ya Yanga ilimwona na kumsajili na kuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa timu hiyo.

Miongoni mwa wachezaji aliowakuta na kucheza nao ni Issa Athumani (marehemu), Willy Mtendamema, Willy Martin ‘Gari Kubwa’, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’.

Wengine ni Method Mogela ‘Fundi’ (marehemu), Mwanamtwa Kiwhelo, David Mwakalebela, Kenneth Mkapa, Stephen Nemes, Riffat Said (marehemu), Edibily Lunyamila, Said Mwamba ‘Kizota’ na Jumanne Shengo.

Mmachinga ndiye Mtanzania pekee anayeshikilia rekodi ya ufungaji wa mabao mengi Ligi Kuu Tanzania Bara. Nyota huyo alifanikiwa kufunga mabao 26 kwa msimu wa 1999/2000 akiwa na klabu ya Yanga, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo hii.

Pamoja na mpachikaji mabao huyo kuichezea Yanga kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka saba, pia mwaka 2001 akiwa na klabu ya Simba aliibuka mfungaji bora katika michuano ya Kombe la Tusker.

Mpachikaji mabao huyo aliongoza katika michuano hiyo kwa kufunga mabao manne akifuatiwa na winga aliyekuwa anachezea timu ya Yanga, Edibily Lunyamila, ambaye alifunga mabao matatu.

Kutokana na kuwa kinara katika ufungaji mabao katika michuano hiyo, Kampuni ya Bia Kibo Breweries iliyoandaa michuano hiyo, ilimzawadia fedha taslim Sh milioni 1.5.

13.EDIBILY LUNYAMILA

Winga wa kushoto Lunyamila, ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga waliocheza fainali dhidi ya Club Sports Villa ya Uganda, mwaka huo wa 1993 na timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku yeye akifunga bao la pili.

Mkongwe huyo alisifika kwa aina ya uchezaji wake, kwani alikuwa na kasi sana, chenga za maudhi na umahiri mkubwa wa kupiga krosi zilizokuwa zinawafikia washambuliaji wa kati ambao walikuwa wanafunga mabao. 

Nyota huyo alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka kuwa ana kipaji hicho cha kasi na uwezo mkubwa wa kupachika mabao mwaka 1992, wakati alipokuwa akichezea timu ya Biashara ya Shinyanga ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu).

Winga huyo teleza wakati akichezea timu ya Biashara ya Shinyanga alikuwa akiwanyanyasa vilivyo mabeki waliokuwa akikabiliana nao kutokana na kasi yake hiyo, huku ‘akiwalamba’ chenga za maudhi, kupiga krosi na wakati mwingine alikuwa anakwenda mwenyewe langoni kupachika mabao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*