googleAds

Mastaa walivyovinjari ujenzi wa reli ya kisasa, Tanasha atajwa Diamond kutokuwepo

NA JEREMIA ERNEST

ALHAMISI wiki iliyopita mastaa katika sekta ya sanaa na michezo nchini, walipata fursa ya kuvinjari ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Ruvu, mkoani Pwani.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutaka kuwaonyesha wasanii kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli, katika kuboresha miundombinu ya usafiri nchini, kwani reli hiyo ikikamilika watu wataweza kusafiri na kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa saa tatu.

BINGWA liliambatana na mastaa hao kutoka Stesheni ya Kamata kuanzia majira ya saa tatu asubuhi, lengo likiwa ni kufika Morogoro, tukiongozwa na Makonda na mratibu wa safari hiyo, Steve Nyerere.

VITUKO VYATAWALA

Katika ziara hiyo iliyokuwa na furaha kwa kila msanii, mwanamichezo na wanahabari waliopanda treni hasa wale waliotumia usafiri huo kwa mara ya kwanza toka wazaliwe, burudani zilizoambatana na vituko zilitawala.

Kwani ndani yake kulikuwa na mchanganyiko wa wasanii wa Bongo Fleva, filamu, wanamuziki wa dansi wa Tanzania na Kongo, Taarabu, wacheza mpira wa zamani na wengineo wengi waliofurahi kukutana na kusafiri pamoja kama familia.

WASANII WAVAMIA JIKO LA MUUZA SAMAKI

Ilipofika saa nane mchana msafara ulikuwa katika Stesheni ya Ruvu, hapo wasanii walishuka kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na ghafla kundi lililokuwa likiongozwa na msanii Shilole, lilifika kwenye nyumba ya mama muuza samaki na kuwanunua wote pamoja na kilo mbili za unga.

 “Najua hamjashiba, sasa ngoja tupike ugali haraka ili tujishibie chakula asilia, nakata kachumbari, Keti anza kukoroga uji nakuja tusaidiane kusonga ugali,” alisikika akisema Shilole.

Baada ya chakula hicho kuiva wasanii walijitokeza kula akiwemo Irene Uwoya, Duma, Omari Tego, Mchungaji  Mashimo, Thea na wengine wengi.

TANASHA ATAJWA KUMSHIKILIA DIAMOND

Miongoni mwa mastaa ambao  walitegemewa kuwamo katika safari hiyo ni Diamond Platnumz, ambaye tetesi zinadai alishindwa kuhudhuria kwa sababu mpenzi wake, Tanasha alikuwa anaumwa huku ikidaiwa kuwa tayari amenasa ujauzito.

Chanzo chetu kimetanabahisha kwamba, Tanasha ambaye ni mtangazaji maarufu nchini Kenya, yupo Bongo kwa muda wa wiki mbili sasa.

BINGWA lilimtafuta Diamond Platnumz bila mafanikio hadi tulipompata meneja wake, Babu Tale ambaye alikuwa kwenye safari hiyo naye akasema: “Siku ile Diamond alikwenda kwenye chombo cha habari kuachia video ya wimbo Tetema, ikabidi nije kumwakilisha.”

Aliongeza kuwa hana taarifa za ugonjwa wa Tanasha ila ni kweli yupo Tanzania na kama ni mjamzito basi hilo ni jambo la heri.

 WANAMUZIKI WAKONGO WAPAGAWA NA SGR

Miongoni mwa wasanii waliokuwamo katika safari hiyo ni wanamuziki wa dansi wenye asili ya Kongo, kama vile Nyosh El Sadaat, Patcho Mwamba, Jimmy Manzaka na wengineo ambao walipagawa na ujenzi wa reli hiyo ya kisasa (SGR).

 “Tupo kwa ajili ya kupongeza mazuri yanayofanyika, tumejipanga kutunga wimbo ambao utaelezea mradi huu mkubwa,” alisema Patcho Mwamba.

SAFARI YAISHIA RUVU

Mpango ulikuwa ni kufika mpaka Morogoro, lakini kutokana na majukumu ya wasanii wengi ilibidi safari iishie Ruvu, mkoani Pwani ila wasanii, wanamichezo na wanahabari walijionea ujenzi wa reli hiyo inayotarajiwa kukamilika miezi 10 ijayo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*