Mastaa hawa wapo wapo tu Man Utd

LONDON, England

KWA sasa timu ya Manchester United inaonekana kuzinduka baada ya kuanza vibaya msimu huu ikiwa chini ya kocha, Jose Mourinho.

 Mreno huyo alikiongoza kikosi hicho kuwa na matokeo mabaya katika historia ya klabu hiyo mpaka timu hiyo ilionesha kiwango kibovu dhidi ya Liverpool, kilisababisha afukuzwe na nafasi yake ikachukuliwa na nyota wake wa zamani,  Ole Gunnar Solskjaer.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Mourinho, baada ya kukabidhiwa timu hiyo kwa haraka ilianza kufanya vizuri kwa kuichapa Cardiff City kwa mabao matano idadi ambayo ni ya kwanza kubwa kwa mashetani hao wekundu kuipata tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson.

 Mbali na hilo, kiwango cha Man United kinazidi kuimarika kutoka nafasi ya sita mpaka ya tano na vilevile huku ikiwa bado inapigana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.

Chini ya Solskjaer, klabu hiyo bado haijaonja kipigo na huku wachezaji wake kama vile Marcus Rashford na Paul Pogba, wakizidi kutakata baada ya kushindwa kufanya vizuri chini Mourinho.

 Licha ya timu hiyo na baadhi ya wachezaji kuzidi kufanya vizuri, lakini kuna wengine ambao hali zao ni mbaya na wanatafakari kuondoka Old Trafford kabla ya msimu ujao kuanza.

Wafuatao ni wachezaji wanne ambao hali zao ni tete chini ya kocha huyo wa muda.

 4 Matteo Darmian

 Matteo alianzia kibarua chake katika klabu ya AC Milan kabla ya kutimkia  Torino, ikiwa ni bada ya kuzichezea timu za Padova na Palermo zote za nchini Italia.

 Baada ya kucheza kwa kipindi cha misimu minne katika klabu hiyo ya  Torino, beki huyo wa kulia wa timu ya Taifa ya Italia mwaka 2015 alisajiliwa na Manchester United wakati ikiwa chini ya  Louis Van Gaal.

Wakati Damian alipoanza kibarua hicho na Man United, alikuwa akionekana kama atakuwa msaada kwa Antonio Valencia. Hata hivyo, kutokana na mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Muitaliano huyo akajikuta akiondolewa kwenye kikosi cha kwanza na hivyo kuwa msugua benchi.

 Wakati msimu huu unaanza zilikuwapo tetesi zikimhusisha kwamba ataondoka kwenye klabu hiyo, lakini majeraha aliyokuwa nayo yakamfanya aamue kubaki.

Endapo ataaondoka majira ya joto yajayo, basi Darmian ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake alioutoa na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la FA, EFL na ubingwa wa Ligi ya Europa.

 3. Antonio Valencia

Si mashabiki wengi wanaoweza kusema  kwamba Valencia hakuifanyia kitu chochote klabu hiyo tangu ajiunge nayo mwaka 2009 akitokea katika timu ya  Wigan.

 Kutokana na kiwango alichokionesha staa huyo raia wa Ecuado, kilimfanya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson, kumkabidhi jezi namba 7, baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na kunyakua tuzo ya Sir Matt Busby msimu wa 2011-12.

Hata hivyo, mshindi huyo mara mbili wa ubingwa wa Ligi Kuu England, alijikuta akirejeshewa jezi yake ya zamani namba  25, baada ya kushindwa kufanya vizuri msimu wa 2012-13.

Kwa miaka kadhaa, Valencia jina lake limekuwa halikosekani katika kikosi cha kwanza na Jose Mourinho alikuwa akimtaja kama beki bora wa kulia duniani.

Hata hivyo, tangu awasili Ole kwenye klabu hiyo, Antonio ameshindwa kupata nafasi hiyo kwenye kikosi cha kwanza na huku majeraha yakizidi kumzibia zaidi.

Wakati wa usajili wa dirisha dogo la Januari mwaka huu, zilikuwapo tetesi za kwamba angeondoka lakini itashuhudiwa nahodha huyo wa Manchester United akiumalizia msimu huu klabuni hapo ingawa anaweza kuondoka ukimalizika kutokana na kukosa namba mara kwa mara.

 2 Juan Mata

 Licha ya kumuorodhesha nyota huyo katika orodha hii ya wachezaji ambao hawajui hatima yao, kunaweza kuzua maswali mengi lakini kwa sasa Mhispania huyo ameshaonekana kutokwa kwenye mipango ya Ole Gunnar Solskjaer.

Juan ni kati ya wachezaji waliosajiliwa wakati timu hiyo ikiwa chini ya David Moyes na mwenzake, Fellaini ambaye aliondoka Januari mwaka huu.

 Katika kipindi hicho, Man United ilikuwa ikihitaji wachezaji wabunifu na  Mata alikuwa mchezaji mbadala wa kutatua tatizo hilo na ushirikiano wake  Rooney ndiyo iliyokuwa silaha iliyoiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la FA ikiwa chini ya Louis Van Gaal.

Ujio wa Mourinho katika klabu hiyo ilikuwa ikionekana kuwa ndio mwisho wa staa huyo kuonekana katika kikosi hicho, lakini kocha huyo alikuwa akimpa nafasi walau za kucheza ingawa mara nyingi alikuwa akianzia benchi.

Kuanzia kipindi hicho cha Mourinho na sasa Solskjær, Mhispania huyo anaonekana kuchanganyikiwa na ndio maana mpaka sasa hajasaini mkataba mpya na hali hiyo ikiendelea inaweza ikashuhudiwa akiondoka majira ya joto yajayo ili akasake mahali pa kucheza mara kwa mara.

  1 Marcos Rojo

Marcos Rojo alisajiliwa na Manchester United akitokea katika timu ya Sporting CP mwaka 2014 kwa ada ya pauni milioni 16.

 Baada ya kuwasili katika klabu hiyo nyota huyo raia wa Argentina, alianza kucheza kama beki wa kushoto kabla ya baadaye kuhamishiwa nafasi ya beki wa kati.

Rojo mara zote alikuwa beki wa kuaminika na alionesha ushirikiano mzuri na Phil Jones chini ya Jose Mourinho.

Hata hivyo, tatizo la majeraha ndilo linalomgharimu Marcos na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

 Kwa mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa ni wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya  Valencia, lakini tangu kipindi hicho amekuwa nje ya uwanja akiwa majeruhi.

Kutokana na hali hiyo, itailazimu Man  United kujiandaa kusaka beki wakati wa usajili wa majira ya joto yajayo na itahitaji kuwapiga bei nyota wake kadhaa ili kupata fedha za kujitosa sokoni na Rojo anaweza akapitiwa na panga jilo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*