googleAds

MARIANO DIAZ MRITHI WA RONALDO ALIYEIVAA KIBISHI JEZI NAMBA 7

MADRID, Hispania

WAKATI Real Madrid ikielekea katika mchezo wake wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Roma juzi, macho na masikio ya mashabiki wa kandanda ulimwenguni yalikuwa kwa dogo huyo.

Wengi walitaka kujua atakachokifanya Mariano Diaz akiwa ndiye mchezaji aliyekabidhiwa jezi namba 7 ya staa Cristiano Ronaldo, aliyetimkia Juventus.

Diaz, aliyetokea benchi katika mchezo huo, ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Roma, akifunga bao kwa shuti kali katika dakika ya 90.

Je, ni yapi usiyoyajua kuhusu nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mzaliwa wa Barcelona, Hispania?

  1. Straika huyo aliwahi kushindwa kupata nafasi Madrid na ndipo alipouzwa Lyon ya Ligi Kuu ya Ufaransa Ligue 1, kabla ya kurejea Santiago Bernabeu. Akiwa Lyon, alicheza mechi 34 na kufunga mabao 18.
  2. Kurejea kwake Madrid kulikuwa na changamoto kubwa kutoka kwa Sevilla, ambao tayari walishazungumza na Lyon na kukubali kuweka mezani euro milioni 8 (zaidi ya Sh bil. 21 za Tanzania).
  3. Bado baadhi ya mashabiki wa Madrid hawakubaliani na uamuzi wa klabu hiyo kumpa jezi namba 7 kwa kuwa ina heshima kubwa klabuni hapo. Mbali ya Ronaldo, ilivaliwa na wakongwe Raul, Butragueno na Juanito.
  4. Kupandishwa kwake kikosi cha kwanza pale Madrid, kabla ya kufeli, kulisababishwa na kocha Zinedine Zidane, ambaye alimpandisha kutoka kikosi cha vijana kwa lengo la kuchukua nafasi ya Karim Benzema, aliyekuwa majeruhi.
  5. Msimu uliopita, jumla ya mashuti yake saba yaligonga mwamba. Kwa kufanya hivyo, aliwapiku wachezaji wote wa Ligi Kuu ya England, akiwamo aliyekuwa kinara wa kufanya hivyo, Harry Kane (6).
  6. Kama ilivyo kawaida ya mastaa wengi wa soka, Diaz pia ni shabiki mkubwa wa mitandao ya kijamii. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa kwa Instagram pekee, ana wafuasi wapatao 950,000.
  7. Licha ya kufunga bao juzi, changamoto kubwa aliyonayo Diaz ni kuhakikisha anawapiku Gareth Bale, Benzema na Asensio katika vita ya kuingia first eleven ya kocha wa sasa wa Madrid, Julen Lopetegui.
  8. Ukiacha Sevilla ya La Liga, kabla ya kurejea Madrid, saini ya nyota huyo ilikuwa dili Ligi Kuu ya England, akiwaniwa na klabu za Everton na West Ham United.
  9. Mchezaji huyo ni kipenzi cha Rais wa Madrid, Florentino Perez, na bosi huyo ndiye aliyeshinikiza arudi klabuni hapo. Tangu mwaka jana, Perez alitaka kumrudisha, lakini aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Zinedine Zidane, hakuona umuhimu wake.
  10. Kama ilivyo kawaida, ni nadra kusikia mchezaji wa Madrid akiwa shabiki wa Barcelona. Iko hivyo pia kwa Diaz, ambaye licha ya kuzaliwa Catalunya, hana mpango nayo.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*