googleAds

Mapumziko ya Corona yasiondoke na viwango vya wachezaji Bongo

Zainab Iddy

KWA sasa Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa siku 30 kuanzia Machi 18, mwaka huu, ili kupisha mapambano dhidi ya virusi vya Corona ambavyo ni janga la Dunia.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, virusi hivyo huathiri mfumo wa hewa, hivyo lazima tahadhari zichukuliwe kwa kufuata kanuni za afya.

Kwa kutambua janga hilo la Dunia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa agizo la kusitisha shughuli zote zitakazoleta mikusanyiko ya watu, ikiwemo michezo.

Katika michezo, soka limeguswa kwa ligi zote kusimama, kipindi ambacho Ligi Kuu Bara ilikuwa inaelekea ukingoni, ambapo robo tatu ya michezo ilishachezwa.

Kuna mambo yalikuwa yanatokea ndani ya Ligi Kuu, lakini kubwa ni lile la hekaheka ya kujinasua kushuka daraja na nyingine zikipigania kupanda kutoka ligi Daraja la Kwanza.

Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu, timu sita zipo katika hali tete, hasa ikiwa itatokea msimu kuhitimishwa leo.

Timu hizo ni KMC iliyopo nafasi ya 15 kwa pointi 33, Ndanda FC ina pointi 31 ikiwa nafasi ya 16, zote zikiwa zimecheza mechi 29 na kusaliwa na michezo tisa pekee.

Endapo ligi itaisha zikiwa nafasi hizo, zitapata nafasi ya kwenda kucheza mechi za ‘Play Off’ na zile za Ligi Daraja la Kwanza zitakazomaliza katika nafasi ya pili Kundi A na B.

Nyingine ni Mbeya City iliyo nafasi ya 17 kwa pointi 30, Alliance ya 18 kwa pointi 29. Mbao iko nafasi ya 19 ikiwa na pointi 22, ikiwa imebakiza mechi 10, huku Singida United ikiwa nafasi ya 20 kwa pointi 15 ikiwa imecheza mechi 29.

Nne za mwisho katika msimamo ikiwa zitashindwa kupiga hesabu vizuri basi mkono wa kwa heri unazihusu kutokana na ukweli kwamba msimu huu zinashuka nne.

Tayari inafahamika mwenendo mzima wa ligi umekuwa na matatizo na baadhi yake ni waamuzi kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka, jambo lililopunguza ladha iliyozoeleka katika ligi.

Kwa upande wa ligi daraja la kwanza, nako kila mmoja anataka apande daraja ili kushiriki Ligi Kuu Bara, hivyo kuwapo kwa upinzani mkali ukizingatia msimu huu ni mbili pekee zitapata nafasi ya kupanda moja kwa moja ambazo ni zile zitakazongoza makundi yao.

Kikubwa kinachotakiwa kufanyika kwa ligi zote ni timu kupambana na waamuzi kufuata sheria 17 ili kuepuka mambo yasiyofaa katika soka.

Inaumiza kuona kwenye kiwanda cha kutengeneza wachezaji wajao kunakuwa na madudu mengi yasiyokuwa na tiba licha ya kelele nyingi zinazopigwa na wadau.

Aidha, hakuna shaka kuwa mapumziko ya ghafla yaliyojitokeza yatakuwa na athari katika soka la Tanzania, hasa upande wa uchumi, nyanja muhimu kwa mpira wa miguu duniani.

Mbali ya hilo, wapo wachezaji watakaotumia kipindi hiki cha mapumziko kufanya mambo yatakayoathiri afya zao.

 Ni vema wakajiepusha na hilo, ikiwamo kukwepa vyakula vitakavyowaongezea uzito.

Wachezaji wanaojitambua wanafahamu kuwa hiki ni kipindi cha kufuata programu walizopewa na makocha wao ili kurudi na kasi itakayowapa nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*