MAPIGANO MATAKATIFU – 49 –

Ilipoishia

Msichana Nina akiwa nyumbani aliletewa taarifa na rafiki yake kuwa malkia Zayana amewaruhusu watu wote wapandishe mlimani kwenda kumwona chifu. Taarifa hiyo ilimshtua Nina aliyekuwa amemkumbuka mpenzi wake Tela kiasi cha kumkondesha mwili.

Hakuamini kabisa, kwanza alikuwa na maswali mengi maana yeye alijua kuwa Tela alikuwa Bitapor.

SASA ENDELEA…

Swali hilo lilibaki moyoni mwake maana ilikuwa ni siri kati yake yeye na Tela, lakini alishangaa kusikia atakuwa mlimani wakati ilikuwa ni miaka sita tokea alipoondoka kwenda Bitapor.

*******

Furaha ilikuwa kubwa kwa wananchi wa Pangawe ambao nao walikuwa wakiamini chifu wao alikuwa akiishi mlimani kwa miaka yote hiyo. Hata viongozi wengi wa ardhi hiyo walijua vivyo hivyo.

Siku ya Jumatano asubuhi, maelfu ya watu walianza kuupanda mlima Noria mlima ulioitwa mlima wa Mungu uliokuwa na misitu mirefu na mapori.

Ni wananchi wachache sana waliobaki chini kwenye makazi yao, wao hawakutaka kwenda, kwa sababu walihofia usumbufu watakaopata kutokana na idadi kubwa ya watu iliyopandisha huko. Wengine bado walikuwa waoga wakiogopa wanyama wakali hasa nyoka ambao ndio walinzi wakuu wa mlima huo.

Walipofika katikati ya mlima, kamanda wa jeshi aliwatangazia wananchi wote kupandisha tena hadi juu kidogo ili wakalifikie eneo la ibada, ambapo chifu atakuwa huko akiongoza ibada pamoja na viongozi wa dini.

Wananchi walipandisha tena hadi eneo waliloliita Gazavela lililokuwa kilomita 50 kabla ya kufika katika kilele cha mlima huo, eneo lililokuwa maalumu kwa ibada kuu. Baridi ya eneo hilo ilikuwa ya juu kidogo kulinganisha na ile ya maeneo ya katikati ya mlima.

Mamia ya watu walikusanyika hapo wakimsubiri Tela aliyekuwa ndani ya nyumba maalumu ya eneo hilo. Kila jicho la mwananchi lilikuwa na hamu ya kumuona chifu wao aliyeishi katika mlima huo kwa zaidi ya miaka mitano.

Malkia Zayana naye ilimlazimu kupandisha malimani akiwa amebadili wazo lake la kuonana na Tela huko huko akihitaji asishuke katika miliki yao. Alibebwa kwenye kiti maalumu na askari wanne akiwa na msafara wa viongozi na askari wengine.

********

Tela alitoka nje ya nyumba hiyo akiwa amevaa mavazi ya kiasili kama ambavyo alikuwa akivaa siku zote. Watu walipomuona, walishangilia kwa nguvu huku wangine wasiamini kama walikuwa wakimuona kiongozi wao. Ukuaji wa haraka wa kimo chake, uliwashangaza wengi, watu waliwabeba watoto wao mabegani ili wamuone chifu wao.

Tela alisimama mbele ya umati wa watu akiwa na tabasamu zuri ajabu. Alinyoosha mkono mara moja kitendo kilichoongeza nguvu ya wananchi katika kupiga kelele za kushangalia.

Viongozi mbalimbali pamoja na wazee wachache wa baraza nao walikuwa mbele, kiongozi Sadamu Kabia naye alikuwepo. Alipomuona Tela moyo wake ulijawa na chuki isiyopimika. Nafsi yake iliwaka hasira huku ikijilaumu kwa kushindwa kumuua kijana huyo.

Alijiuliza alishindwaje kumuua tokea alipokuwa mdogo, maana aliona kuna ugumu kidogo kwa wakati huo kwa kuwa Tela alishakuwa anakwenda kuwa mtu mzima, maana alibakiza mwaka mmoja tu awe na umri wa miaka 18.

Zayana aliwasili eneo hilo na kukuta umati mkubwa wa watu ukishangilia mbele ya mwananye. Aliwaamuru askari kumshusha chini, alishuka kwenye kiti cha kubebwa na kuanza kutembea.

Alifika hadi mbele ambapo mwanaye yupo, macho yake yalimuona mtoto wake aliyekuwa amekua kupita kawaida, hakuamini alihisi anaota. Kwani hata yeye aliishi kwa zaidi ya miaka mitano bila kumuona kipenzi chake.

Lakini hakutakiwa kuonyesha shauku kali mbele ya wananchi na viongozi wote maana watu wangehoji kuwa inamaana hakuwa akipandisha mlimani kumtazama mtoto wake. Hata Tela naye hakutakiwa kuonyesha amemkumbuka sana mama yake, ilitakiwa iwe hivyo ili kuficha juu ya mahali alikokuwa.

Zayana alimsogelea mwanaye akamshika bega kwa mkono wake wa kushoto na mkono mwingine akaushika mkono wa Tela. Walisalimiana kawaida tu kisha Tela aliwageukia tena wananchi wake.

Zayana alikwenda kukaa kwenye kiti. Tela alianza kuwahutubia maelfu ya watu katika eneo hilo la Gazavela kama hotuba yake mpya. Wananchi walikaa kimya kumsikiliza. Alisimama na kusema.

“Japo bado sijapewa mkuki na ngozi ya simba kama mwanzo wa utawala wangu, lakini nitaongea na nyinyi kama nimekwisha kupewa.

Kwanza niwashukuru wananchi wangu kwa uvumilivu wenu mliokuwa mmeuhifadhi kwenye nafasi zenu kwa miaka sita.”

Nini kitaendelea? Usikose Alhamisi


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*