MANJI KUREJEA YANGA…

NA HUSSEIN OMAR

HATMA ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kama atarejea katika klabu hiyo au la itajulikana kesho kwenye Mkutano Mkuu.

Mashabiki wa klabu hiyo ya Yanga wamekuwa na hamasa kubwa tangu jana, baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba mfanyabiashara huyo aliyejiuzulu kuiongoza timu hiyo mwaka jana akidai anatoa nafasi kwa wengine kuongoza, huenda akarejea.

Pamoja na taarifa hizo za kurejea kwake, imedaiwa kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa na mpango wa kuwekeza zaidi ya bilioni 30 kwa Wanajangwani hao.

Yanga iliyumba kichumi baada ya mfanyabiashara huyo kuachia ngazi, lakini habari za kurejea kwake zimekuwa gumzo na kumvutia kila shabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.

Hivyo mambo yote yatakuwa hadharani kesho katika Mkutano Mkuu, utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo, utajadili mambo mbalimbali yanayohusiana na Yanga, huku ajenda kuu ikiwa ni mabadiliko ya kimfumo wa uendeshaji wa klabu.

Taarifa ilizozipata BINGWA, zinasema  mazungumzo kati ya bilionea huyo na viongozi wa juu wa klabu, yamefikia sehemu nzuri na kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa huenda tajiri huyo akawekeza kiasi hicho cha fedha cha bilioni 30 kwa ajili mfumo huo mpya wa uendeshaji.

“Mungu asaidie mambo yaende kama yalivyopangwa na tayari jamaa amekubali kuwekeza bilioni 30. Hivyo tunaomba wanachama waje kwa wingi kwenye mkutano, ’’alisema.

Chanzo hicho kilisema bilionea huyo atakaporejea Jangwani, amepanga kufanya usajili wa nguvu kwa ajili ya kutengeneza timu ya msimu ujao na kupiga panga wachezaji wote ambao msimu huu walishindwa kuwa msaada.

“Jamaa ana mipango mingi sana, ikiwamo kumwaga fedha kwa ajili ya usajili wa nguvu, pamoja na kulipa madeni yote ambayo yaliachwa nyuma na watu ambao walikuwa si waaminifu katika utendaji wao wa kazi,” alisisitiza.

Akizungumzia mkutano huo wa kesho kwa upande wa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alisema maandalizi yote kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika na vigogo wote walioalikwa wamethibitisha kushiriki.

“Maandalizi yote yapo sawa kama nilivyosema hapo nyuma, kuna ‘surprise’ kubwa imeandaliwa, naomba wanachama na wapenzi wa Yanga wajitokeze kwa wingi ili kuja kusikiliza nini kitakachojiri hiyo kesho kutwa (kesho),” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe, ambaye atawaongoza wanachama watakaofika katika mkutano huo.

Naye mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Ally Mayay, alisema hakuna mtu anaeweza kuweka fedha sehemu kisha akawa hana mamlaka nazo katika namna ya kuzitumia na kuongeza kuwa mabadiliko hayaepukiki.

Alisema dhamira ya wanachama ni kuona timu yao inashinda na kutwaa mataji,  hivyo kumpata mwingine mtu anaeweza kutumia  mamilioni katika soka kwa sasa si kazi rahisi.

 

“Ni jambo la furaha sana kama kweli atarejea, ni ngumu kwa sasa kupata mtu kama huyu, mimi nasema kurudi kwake kutarudisha heshima ya klabu ,” alisema Mayay.

Pamoja na Mayay, nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema amefurahishwa na taarifa za kurejea kwa bilionea huyo na kuwataka wapenzi na mashabiki wa Yanga kukaa mkao wa kula.

“ Ni jambo zuri sana, tumepitia wakati mgumu sana, Mungu kasikia kilio chetu kama kweli anarudi nina imani tutabeba mataji yote msimu ujao,” alisema Cannavaro.

Yanga imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji, Mei mwaka jana.

Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini akapata upinzani mkali na kuamua kuachana na mpango huo.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*