MANCHESTER CITY KUIVAA LIVERPOOL BILA GUNDOGAN

MANCHESTER, England


 

TIMU ya Manchester City itaifuata Liverpool wikiendi hii kwenye mchezo mkali wa Ligi Kuu England bila uwepo wa kiungo wao Mjerumani, Ilkay Gundogan, anayesumbuliwa na maumivu ya msuli wa paja.

Gundogan alionekana kuugulia maumivu alipokuwa akifanyiwa mabadiliko katika kipindi cha pili cha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Hoffenheim, uliochezwa mapema wiki hii.

Kutokana na hali hiyo iliyomkumba Gundogan, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na kiungo mwenzake, Bernardo Silva dhidi ya Hoffenheim, huenda akaukosa mtanange wa kukata na shoka dhidi ya Liverpool.

Imeripotiwa kuwa Gundogan, mwenye umri wa miaka 27, atakuwa chini ya uangalizi makini wa madaktari wa klabu hiyo ili kuchunguza ukubwa wa tatizo lake hilo.

Kiungo mwingine wa City aliyekuwa majeruhi, Kevin De Bruyne, alianza mazoezi wiki hii, baada ya kupona, lakini kocha wake, Pep Guardiola, alisema hataharakisha kumchezesha wikiendi hii.

De Bruyne alianza mazoezi Jumatatu ya wiki hii, baada ya kupita wiki tano za kuuguza jeraha la goti, na kurudi kwake mapema kuliamsha matumaini ya mashabiki wa City kwamba ataweza kucheza dhidi ya Liverpool.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*