Man United wachapwa mechi ya tatu mfululizo

LONDON, England

Manchester United wamepoteza mechi yao ya tatu mfululizo, baada ya kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Watford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa jana.

Etienne Capoue alifunga bao lake la nne msimu huu katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Vicarage Road, kabla ya Marcus Rashford kusawazisha baada ya mapumziko.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Walter Mazzarri ya kumwingiza Juan Camilo Zuniga yaliibeba Watford, baada ya mchezaji huyo kufunga bao kwa mpira wake wa kwanza kugusa dakika saba tangu aingie dimbani, kisha Troy Deeney aliongeza bao lingine kwa penalti kufuatia Zuniga kuchezewa vibaya na Marouane Fellaini.

Kipigo hicho kwa Man United, inayonolewa na kocha Jose Mourinho ni cha tatu ndani ya siku nane, baada ya kufungwa 2-1 na Manchester City katika mchezo wao wa Jumamosi iliyopita, kabla ya kupokea kichapo kingine kwenye mchezo wa Ligi ya Europa dhidi ya Feyenoord, Alhamisi iliyopita.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mourinho kupoteza mechi tatu mfululizo tangu Agosti 2006, alipokuwa anainoa Chelsea kwa mara ya kwanza.

Wenyeji hao wamewafunga United kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 kupita na mshambuliaji wao, Odion Ighalo alipoteza nafasi ya wazi baada ya shuti lake kutoka nje.

Nafasi hiyo ya Ighalo ilitokea baada ya mlinda mlango wa Man United, David de Gea kugongana na beki wake, Chris Smalling.

De Gea aliokoa shuti la Deeney, kabla ya United kupoteza nafasi yao ya kwanza, baada ya Zlatan Ibrahimovic kupiga shuti lake nje akiwa umbali wa yadi sita.

Paul Pogba, akicheza pamoja na Wayne Rooney na Fellaini kwenye safu ya kiungo chenye wachezaji watatu, aligonga mwamba baada ya shuti lake la mbali.

Anthony Martial aliporwa mpira jirani na eneo lao la hatari na Daryl Janmaat kupiga krosi iliyounganishwa na Capoue.

Martial hakurudi tena uwanjani baada ya kuumia alipogongana na Janmaat wakati anapokonywa mpira na nafasi yake ilichukuliwa na Ashley Young kabla ya mapumziko.

United walisawazisha kwa bao la Rashford, ambaye alianza tena kwenye kikosi hicho baada ya kucheza dhidi ya Feyenoord, alifunga bao hilo kuunganisha krosi ya Ibrahimovic.

Man United walionekana kupagawa na wachezaji wake, Rooney, Memphis Depay na Fellaini kuonyeshwa kadi za njano dakika za mwisho za mchezo huo, ambapo Watford waliongeza bao la pili lililofungwa na Zuniga, kabla ya mwamuzi

Michael Oliver kuwapatia Watford penalti iliyofungwa na Deeney.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*