MAMBO NI MOTO YANGA

*Mkwassa atua na timu Mtwara, awapa habari njema mashabiki

*Yondani arudishiwa kitambaa; Balinya, Sibomana roho kwatu

NA ASHA KIGUNDULA

MAMBO ni moto ndani ya Yanga kwani ikiwa ni saa chache tangu kutimuliwa kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, kikosi cha Wanajangwani hao kimetua Mtwara kikiwa na ari na nguvu mpya chini ya Charles Boniface Mkwassa atakayesimamia ‘shoo’ watakapocheza na Ndanda ya huko kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mkwassa aliongozana na timu jana kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara, tayari kukiongoza kikosi chake kusaka pointi tatu muhimu katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa Mkwassa tangu alipotangazwa juzi na uongozi wa Yanga kuchukua nafasi ya Zahera aliyefungashiwa virago kutokana na madai ya mwenendo usioridisha wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Akizungumza na BINGWA akiwa njiani jana kwenda Mtwara akiwa na vijana wake, Mkwassa alisema japo ni mapema mno kuzungumzia matarajio yake ndani ya kikosi hicho, lakini iwapo atapewa ushirikiano, mashabiki wa Yanga watafurahi tu.

Alisema pamoja na mambo mengine, anatamani kuona mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanjani kama ilivyokuwa kawaida yao enzi zake akiinoa timu hiyo ili kuwapandisha mzuka wachezaji.

“Nimepewa jukumu la kuwa na timu ya Yanga katika kipindi hiki kigumu cha kutoka kwenye michuano ya Kimataifa, siwezi kusema nitaifanyia nini Yanga kwa sababu naona ni mapema sana, lakini ninachoomba ushirikiano uwepo tuweze kuifanyia makubwa Yanga,” alisema Mkwassa.

Aliongeza: “Mimi si mgeni Yanga, nimefanya kazi nikiwa kama mchezaji, kocha na kiongozi wa juu pia, hivyo ninachohitaji ni ushirikiano kutoka kwa mashabiki, wanachama na viongozi ili tuweze kwa pamoja kufika pale ambapo kila mmoja wetu anapatamani.”

Alisema anafahamu kuwa wachezaji wa timu hiyo watakuwa wamechanganyikiwa kutokana na mabadiliko yaliyotokea, akiwataka kutuliza akili na kila mmoja kutimiza majukumu yake yaliyompeleka Yanga.

Mkwassa alisema atahakikisha anazungumza na wachezaji wake wote ili kuwaweka sawa na kuwakumbusha majukumu yao, akiamini kwa kufanya hivyo, atarejesha amani na umoja miongoni mwao kwa manufaa ya timu na wao wenyewe kwa ujumla.

Yanga itaivaa Ndanda FC kesho ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa na Pyramids ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupokea kipigo cha jumla cha mabao 5-1.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ilifungwa mabao 2-1, kabla ya mwishoni mwa wiki iliyopita kulala kwa mabao 3-0 nchini Misri na kuaga michuano hiyo.

Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa Kelvin Yondani, yupo mbioni kurejeshewa kitambaa chake cha unahodha ikiwa ni baada ya kuvuliwa wakati wa maandalizi ya msimu huu.

Zahera alimvua Yondani cheo hicho na kumpa Papy Tshishimbi baada ya beki huyo wa kati kuchelewa kujiunga na timu mjini Morogoro akishinikiza kulipwa kwa stahiki zake.

Habari kutoka ndani ya Yanga zilizolifikia BINGWA jana, zinasema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwa cheo hicho kimekuwa ni kizito kwa Tshishimbi.

“Uamuzi huu haujafikiwa kwa kuwa mwalimu Zahera ametimuliwa, hapana…bali imeonekana kitambaa cha unahodho ni kizito kwa Tshishimbi, ameshindwa kukitendea haki. Toka amekabidhiwa, hakuna mabadiliko yoyote katika kiwango chake, kimekuwa kikishuka badala ya kupanda.

“Lakini hata sifa ya uongozi (Tshishimbi) hana, ni tofauti na Yondani, ana msimamo na nguvu ya uongozi na ni muhamasishaji kwa nadharia na vitendo awapo uwanjani,” alisema mtoa habari wetu huyo.

BINGWA lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli ili kuthibitisha juu ya mpango huo, lakini muda wote simu yake ilikuwa haipatikani hadi jana jioni.

Wakati huo huo, straika wa Yanga, Juma Balinya ameonekana kufurahishwa na mabadiliko ya benchi la ufundi yaliyofanywa na uongozi wa klabu hiyo baada ya kutemwa kwa Zahera na nafasi yake kuchukuliwa na Mkwassa.

Saa chache baada ya kutangazwa kwa mabadiliko hayo, katika ukurasa wa mtandao wake wa Instagram, Balinya aliposti picha ya kocha wa timu ya Taifa ya Ujerumani, Joachim Low akiwa ameonyesha dole gumba kuashiria kukubaliana na jambo fulani.

Tukio hilo lilitafsiriwa Balinya kuunga mkono kutimuliwa kwa Zahera ambaye inafahamika hakuwa akifurahishwa naye kutokana na kitendo cha kocha huyo ‘kumchomesha mahindi’.

Mbali ya Balinya, Patrick Sibomana naye hakuwa na wakati mzuri katika siku za hivi karibuni, akiishia benchi kabla ya mwishoni mwa wiki iliyopita kupewa nafasi walipovaana na Pyramids na kuonyesha kiwango kizuri.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*