MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU ‘LASS’ DIARRA

PARIS, Ufaransa

SIKU chache zilizopita, uongozi wa klabu ya PSG ulitangaza kukamilisha usajili wa kiungo mkongwe, Lassana Diarra.

PSG wamemuona Mfaransa huyo kuwa ni mtu sahihi wa kuitumikia safu yao ya kiungo na wamempa mkataba wa miezi 18.

‘Lass’, kama mashabiki wengi wa soka wanavypenda kumwita, alikuwa mchezaji huru tangu alipoachana na Al Jazira ya Abu Dhabi Desemba, mwaka jana.

Hata hivyo, huenda haya ni mambo ambayo hukuyajua kuhusu mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid, Chelsea na Arsenal, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32.

  1. Akiwa mdogo, klabu kadhaa zilimkataa, zikisema ni mfupi na mwepesi, hivyo ‘asingetoboa’ katika soka. Mfano, Nantes walimtolea nje na baadaye Le Mans nao walikataa kumchukua.
  2. Aliyempeleka Chelsea ni mtaalamu Gwyn Williams, aliyekuwa skauti wa Chelsea, ambaye pia ndiye aliyemuibua John Terry. Lakini pia, akiwa Stamford Bridge kwa miaka 27, Williams aliweza kumsajili mpachikaji mabao Andre Flo.
  3. Alipotua Chelsea mwaka 2005, alinunuliwa kwa lengo la kuziba pengo la Mfaransa mwenzake, Claude Makelele, ambaye umri ulikuwa umemtupa mkono. Hata mashabiki wa soka nchini Ufaransa walimpachika jina la ‘Makelele mpya’.
  4. Mwaka 2015, alifiwa na binamu yake wa kike aitwaye Asta Diakite, aliyepoteza maisha katika shambulio la kigaidi lililotokea jijini Paris. Tukio hilo lilitokea siku ambayo Diarra alikuwa mzigoni katika mchezo kati ya Ufaransa na Ujerumani.
  5. Licha ya kucheza katika klabu nyingi barani Ulaya, Diarra, ambaye alitua Real Madrid akitokea Portsmouth, ni shabiki mkubwa wa Marseille, ambayo alianza kuifuatilia tangu akiwa mdogo.
  6. Diarra alipoitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa kilichokwenda kucheza fainali za Euro 2016, hakuwa amecheza soka kwa miezi 15, baada ya kuachana na Lokomotiv Moscow ya Urusi.
  7. Miongoni mwa timu zilizoshindwa kufaidika na huduma ya kiungo huyo ni Chelsea. Kwa kipindi chote cha miaka miwili Stamford Bridge, Diarra alicheza mechi 13 pekee za Ligi Kuu England.
  8. Nyota huyo, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa goti, anatajwa na jarida la Forbes kuwa na utajiri wa Dola za Marekani milioni 49, ambazo ni zaidi ya Sh Bil 100 za Tanzania.
  9. Diarra, ambaye alikuwa anawaniwa pia na Jose Mourinho wa Manchester United, anatua PSG kumsaidia majukumu Thiago Motta, mwenye umri wa miaka 35. Lakini pia, atakuwa msaidizi wa Adrien Rabiot katika idara ya kiungo.
  10. Muumini huyo wa Dini ya Kiislamu aliwahi kutozwa faini ya Pauni milioni 6.8 (zaidi ya Sh bil. 21 za Tanzania) baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Lokomotiv Moscow. Aliikacha timu hiyo baada ya kukorofishana na kocha Leonid Kuchuk.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*