MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU DEMBELE

CATALUNYA, Hispania

BAADA ya kumsaka kwa muda mrefu, hatimaye Barcelona wamefanikiwa kukamilisha mpango wa kumsajili fowadi wa Borussia Dortmund, Ousmane Dembele.

Jumatatu ya wiki iliyopita, jumla ya mashabiki 17,814 walifika kwenye Uwanja wa Camp Nou kushuhudia nyota huyo akitambulishwa.

Dembele, aliyenunuliwa kwa euro milioni 105, amekabidhiwa jezi namba 11, iliyokuwa ikivaliwa na staa Neymar, aliyekwenda kujiunga na matajiri wa soka la Ufaransa, PSG.

Je, ni nani huyo Dembele, ambaye licha ya umri wake wa miaka 20, mabosi wa Barca wamemwamini na kumuona mtu sahihi wa kuziba pengo la Neymar?

  1. Dembele kutua Barca ni pigo kwa Real Madrid, waliokuwa wakimfukuzia. Lakini pia, ni habari mbaya kwa Tottenham, Liverpool, Manchester United, Manchester City na Bayern Munich, ambazo pia zimhitaji.
  2. Msimu uliopita, aliifungia Dortmund mabao 10 katika mechi 49. Lakini pia, alishika nafasi ya tatu Ulaya kwa kutoa asisti nyingi (20). Aliweza kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kufikisha asisti tatu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  3. Dembele ndiye mtoto pekee katika familia yao aliyekataa kusoma na kuelekeza akili yake kwenye soka. Wazazi wake waliamua kukubaliana na uamuzi wake huo, huku dada na kaka zake wakiendelea na masomo.
  4. Akiwa mdogo, alivutiwa zaidi na uchezaji wa wanasoka wenye heshima kubwa barani Afrika, Seydou Keita na Frederic Kanoute. Lakini pia, ulikuwa humwambii kitu kwa Ramadel Falcao na Lionel Messi.
  5. Rafiki yake mkubwa kwa sasa ni Pierre-Emerick Aubameyang, aliyekuwa akicheza naye Dortmund. Wanaendesha aina moja ya gari na hata mfumo wa ujenzi wa nyumba zao unafanana.
  6. 6. Kwa mujibu wa mkataba wake wa sasa na Barcelona, nyota huyo atakuwa akivuna kitita cha Pauni 150,000 kwa wiki, ambazo ni zaidi ya Sh 430 za Tanzania.
  7. Licha ya kuwa anaichezea timu ya Taifa ya Ufaransa, Dembele ana asili ya Afrika, kwani mama yake ni mzaliwa wa Mauritania mwenye asili ya Senegal na baba yake ni raia wa Mali.
  8. Dembele amemwajiri mama yake mzazi, Fatimata Dembele, kuwa mmoja kati ya wasimamizi wake katika masuala ya usajili. Kila anaposaini mkataba mpya, bi mkubwa huyo huwa na fungu lake.
  9. 9. Kuitwa kwake kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa kulitokana na Alexandre Lacazette kuwa majeruhi. Hiyo ilikuwa mwaka 2016.
  10. Akiwa Ligue 1 na Rennes, Dembele alichukua tuzo ya Chipukizi Bora, ambayo pia imewahi kuangukia mikononi mwa mastaa Marco Verratti, Eden Hazard, Franck Ribery na Zinedine Zidane. Alipewa baada ya kufunga mabao 12 na kutoa ‘asisti’ tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*