googleAds

MALINZI USIMWONEE SONI KIM PAULSEN

NA HONORIUS MPANGALA

KUNA mambo hayawezekani katika maisha ya kila siku ya binadamu, lakini kwa sababu ya misimamo kwenye soka tuliko sisi inawezekana, sidhani kama waliotalikiana wanaweza kurejeana kirahisi kwa sababu ya maendeleo ya mmoja wao, kinachotokea ni kumwombea mabaya mwenzako avurunde zaidi ili kesho aje kukusujudia na wewe kujiona umepatia kufanya maamuzi.

Mchezo wa soka ni kati ya michezo ambayo ikitokea klabu ikimwacha mchezaji na ikamwona anafanya vizuri alikoenda, watu hufanya jitihada za kumrejesha kundini na kutambua walimwacha kimakosa.

Wako makocha ambao ndoa zao na klabu zilivunjika wakatimuliwa lakini wakifanya vizuri walikoenda hurejeshwa na maisha yakaendelea, watu husahau tofauti zilizojitokeza baina yao.

Wachezaji kama Nemanja Matic, Paul Pogba, Alvaro Morata, David Luiz ni kati ya wachezaji ambao waliuzwa na klabu zao za awali na wakaenda upande wa pili wakaonyesha uwezo mkubwa na baadaye timu walizozihama kujikuta zikiingia mifukoni kuwarejesha, soka halina soni, sisi huwa tunafanya kile tunachokiona ni sahihi.

Wako makocha ambao walitimuliwa katika klabu zao na baadaye wakaweza kurejea na kuzifundisha kwa mara nyingine, Luis van Gaal alitoka Barcelona na akarejeshwa kwa awamu nyingine, Jose Mourinho alitimuliwa Chelsea na akarejea tena, Kenny Daglish aliifundisha Liverpool vipindi viwili tofauti, Guus Hiddink kaifundisha Chelsea vipindi viwili tofauti, Luiz Felipe Scolari aliifundisha Brazil kwa awamu kadhaa akitimuliwa na kurejeshwa, wako makocha wengi ila hao kwa uchache wao.

Tanzania kupitia Shirikisho ya Soka  (TFF), uongozi wake uliwahi kumtimua kocha Kim Paulsen ambaye awali alikuja kama kocha wa vijana, lakini kufanya kwake vizuri akapandishwa hadi kuwa kocha wa Taifa Stars, lakini kitu kilichokuja kutokea mara baada ya Malinzi kuingia madarakani, kilishangaza watu.

Malinzi aliingia na roho ya Kiafrika yaani ya kulipiza kisasi, maana wale walioonekana walikuwa TFF kwa uongozi uliotangulia aliwaengua na yeye kuja na watu wake, pangua pangua ile ikamkumba hadi kocha Kim. Wadau wa soka walisikitishwa na maamuzi yale kwa sababu aliyekuja badala yake Martin “Mart” Nooij Mholanzi aliyekuwa akiinoa Msumbiji, alikuja kutuvuruga kweli kweli, kwa kelele za wadau kutokana na kufanya vibaya akatimuliwa na nafasi yake kupewa Charles Boniface Mkwassa.

Baada ya kujishtukia kwamba aliharibu, Malinzi akamrejesha nchini Kim kama mshauri wa ufundi kwa timu za taifa za vijana.

Kupitia ushauri wa Kim ambaye alihusika sana katika maandalizi ya timu yetu ya vijana Serengeti Boys akiwa bega kwa bega na Bakari Shime, wakawa na kikosi bora sana cha Serengeti Boys.

Mapema mwezi huu TFF ilitangaza kusitisha mkataba wa kocha Mkwassa ambao ulikua unaishia Machi na nafasi yake kupewa Salumu Mayanga. Sitaki kubeza uteuzi huo, nauheshimu uwezo wa Mayanga na kazi zake, kwani klabu alizofundisha ziliweza kuwa na mabadiliko kama vile Tanzania Prisons ya misimu miwili iliyopita.

Kitu pekee ambacho najiuliza, Malinzi anajisikia aibu gani kwa Kim Paulsen kumpa mkataba kuinoa tena Taifa Stars? Ubaya uko wapi? Kwa sababu hakuna asiyejua uwezo wa kocha huyo. Binafsi nilijua kumrejesha Kim kama mshauri wa ufundi ilikuwa tu mbinu ya kutaka kumrejesha, lakini inashangaza kusitishwa kwa mkataba wa Mkwasa bado hakujaweza kumpa nafasi hiyo Kim.

Tunamhitaji sana Kim kwa kipindi hiki ambacho Tanzania tumepangwa katika kundi L kuwania nafasi ya kufuzu kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika mwaka 2019 kule Cameroon, Tanzania imepangwa na timu kama Cape Verde, Uganda na Lesotho.

Katika timu tulizopangwa nazo kiuwezo tumewahi kuzifunga, nazo zimewahi kutufunga nasema hivyo kwa sababu kimpira timu tuna uwezo unaofanana kwa kiasi kikubwa na tunaweza kupamabana nazo na tukapata matokeo ambayo yanaweza kutuweka katika nafasi ya kufuzu AFCON 2019.

Wakati tuko na kocha Mbrazil, Marcio Maximo, tuliwahi kupambana na Cape Verde na tukawafunga wakati mchezo uliotangulia kule kwao walitufunga goli mbili bila, Uganda nao tumekutana mara nyingi, Lesotho mara ya mwisho walitufunga tukiwa tumealikwa katika michuano ya Cosafa tulipopangwa kundi moja na Madagascar na Swaziland.

Kulingana na kundi lilivyo unaweza kulitazama kiuwepesi kama ni rahisi sana kwa Tanzania kupenya, lakini inahitaji jitihada za dhati kuanzia kuwa na benchi zuri la ufundi na si kubabaisha. Stars tunamhitaji sana Kim katika hilo, lakini si Mayanga ambaye alikuwa msaidizi wa Mart Nooij na wakatimuliwa benchi zima.

Watu wa mpira tukikosea tunajisahihisha ndio maana Chelsea wakamrejesha Mourinho na akawapa kombe, ndiyo wachezaji kama Matic wakarejea na kuwa msaada kwa timu sasa inashindikana nini kwa Malinzi kumrejesha Kim?

Kocha Mfaransa Claude Reloy amekuwa mzururaji sana katika timu za Afrika hadi karudia kufundisha kwa nyakati nyingine kwa zile zilizohitaji huduma yake, ilitokea kwa DRC, sasa ni aibu gani aliyonayo Malinzi kwa Kim.

Hakuna haja ya kuwa na soni kama tukitaka kurejesha heshima kwa timu ya taifa walau hata robo tatu ya midadi ya mashabiki kwa nyakati za Maximo, basi mpeni tu Kim timu.

0753449254


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*