Makocha wawasaidie akina Fei Toto, Aiyee, Tshabalala

Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali, aliwahi kukaririwa akisema kuwa wachezaji wa sasa hawajitumi uwanjani tofauti na ilivyokuwa kwa wenzao wa zamani.

Kauli hiyo ya kipa huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, imekuja wakati wapenzi wa soka hapa nchini wakiwa wanaendelea kujiuliza kulikoni timu zetu zinashindwa kufurukuta kwenye michuano ya kimataifa.

Pamoja na timu za Tanzania ikiwamo Taifa Stars kushiriki mara kwa mara kwenye michuano ya kimataifa, ikiwamo ya Afcon 2019 nchini Misri, zimekuwa zikiishia hatua za awali na kutupwa nje.

Angalau Simba msimu uliopita iliweka rekodi ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hali hiyo kwa kiasi fulani imekuwa ikiwakatisha tamaa mashabiki wa soka hapa nchini kuzishabikia timu zao na badala yake kuelekeza macho na masikio yao katika ligi za Ulaya na kwingineko.

Kufanya vibaya kwa timu zetu za klabu na hata zile za taifa, kumekuwa kukipokewa kwa hisia tofauti na wapenzi wa soka hapa nchini, baadhi wakitafsiri kama sehemu ya matokeo ya mchezo wa soka, lakini wengine wakiwashushia lawama viongozi na makocha wa timu hiyo.

Lakini pia, wapo ambao waliwatupia lawama wachezaji kwa madai ya kutojituma wawapo uwanjani na badala yake kutanguliza mbele maslahi binafsi.

Na sasa Pondamali amezidi kuwachongea wachezaji wa Tanzania kwa kudai kuwa wa siku hizi, pamoja na kupewa kila kitu tofauti na zamani, bado wameshindwa kufikia viwango vilivyotarajiwa na wapenzi wa soka hapa nchini.

Alisema iwapo maslahi mazuri wanayoyapata wachezaji wa sasa wangekuwa wanapata wale wa zamani kuanzia miaka ya 1980 mwishoni hadi 1990, soka la Tanzania lingekuwa juu kutokana na jinsi walivyokuwa wakijitolea na kuwa na uchungu na timu wanazozichezea.

Kocha huyo alisema kuwa zamani ilikuwa si mchezo, walikuwa wakijituma mno kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi tofauti na sasa.

Alisema mbali na suala zima la kutokujituma, Pondamali pia amesema wachezaji wa sasa hawana nguvu kama ilivyokuwa enzi zao.

BINGWA tunakubaliana na kauli ya Pondamali, kwani sote tumekuwa tukishuhudia wanasoka wetu wakicheza kilegelege huku wakionekana kutokerwa na matokeo mabaya ya timu zao.

Kwa kiasi fulani, hali hiyo imeonekana kusababishwa na hali ya kubweteka kwa wachezaji wetu hao kutokana na mafanikio kiduchu wanayoyapata.

Lakini pamoja na lawama hizo za Pondamali kwa wachezaji, BINGWA tunaamini nao kama walezi wa vijana wetu hao, wamekuwa wakichangia hilo.

Kila mmoja wetu anafahamu kuwa mara nyingi makocha na viongozi wa timu zetu, wamekuwa karibu na wachezaji kwa kujenga urafiki wa kinafiki wenye lengo la kunufaisha upande mmoja.

Mwisho wa siku, kocha au kiongozi anajikuta akitawaliwa na mchezaji na hivyo kushindwa kumkemea pale anapokwenda kinyume na maadili ya soka.

Kuna mifano michache ya makocha waliowahi kupata mafanikio kutokana na kukwepa mtego wa kufunikwa na wachezaji wake, mmoja wapo akiwa ni Abdallah ‘King’ Kibadeni aliyekuwa akiinoa Simba na hata enzi za marehemu Tambwe Leya, alipokuwa Yanga miaka ya 1990.

Hivyo basi, tutoe wito kwa makocha na viongozi wa timu zetu kutokubali kutawaliwa na wachezaji ama kutokana na ukaribu wao, kiwango cha mchezaji au wingi wa fedha anazolipwa ili mwisho wa siku, waweze kuwa na sauti mbele ya wanaowasimamia pale wanapokiuka taratibu za timu na mengineyo kama hayo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*