googleAds

Makocha watoa ushauri kwa Tanzanite

Glory Mlay

MAKOCHA wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, wametoa ushauri kwa timu ya taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’, kuelekea mchezo utaofuata wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Tanzanite ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kuifunga Uganda jumla ya mabao 4-2, ambapo mchezo wa kwanza, uliochezwa Januari 19, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilishinda mabao 2-1.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa KCCA, Lugogo mjini Kampala, Tanzanite iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kutokana na matokeo hayo, Tanzanite  inatarajiwa kukutana na Senegal, mchezo utakaochezwa Machi 20, mwaka huu, ugenini.

Akizungumza na BINGWA jana, kwa nyakati tofauti,  makocha hao walilipongeza benchi la ufundi la Tanzanite kwa kufanikisha kusonga mbele.

Ezekiel Chobanka ambaye ni Kocha wa timu ya Alliance Girls, alisema  benchi la ufundi la Tanzanite linatakiwa kuboresha safu ya ulinzi ili kuimarika zaidi.

“Kuna uzembe walifanya safu ya ulinzi karibu mechi zote mbili na kusababisha kukoswakoswa mabao mengi, tunamuomba mwalimu (Bakari Shime), aliangalie hilo kwa umakini kuhakikisha wanashinda michezo iliyopo mbele yao,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha wa JKT Queens, Ally Ally, alisema ushindi huu unatokana na ubora wa wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.

“Ni habari njema kwetu kuona timu ya taifa inafikia hatua kubwa kwenye michuano mikubwa kama hiyo, hii inatokana na ubora wa ligi yetu ya wanawake,”

Kocha wa timu ya  Ruvuma Queens, Mohamed Mwamba, alisema wamepiga hatua kubwa katika michuano hiyo na kumtaka  Shime kufuatilia kwa undani Senegal kuwasoma mbinu zao kabla ya kukutana.

Mwamba alisema kufanya hivyo kutampa faida kubwa, kwani atakuwa amebaini staili ya uchezaji wa wapinzani wao  na kufanyia kazi kasoro zao.

Naye Kocha wa Simba Queens, Musa Hassan ‘Mgosi’, alisema Tanzanite ilipofika kwa sasa ni hatua kubwa na wasivimbe kichwa, kwani bado wanasafari ndefu ya kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika  Panama na Kosta Rica.

Alisema anaamini kocha wa timu hiyo, anaweza ndio maana amepewa kikosi hicho, hivyo anatakiwa kufanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika michezo iliyopita.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*