MAKOCHA 10 WANAOVUTA MKWANJA MREFU

 MOSCOW, Urusi    |

KIU ya mashabiki wa soka ulimwenguni kote inasubiri kushuhudia fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika nchini Urusi, mwaka huu.

Jumla ya mataifa 32 kutoka sehemu mbalimbali duniani yatakuwa yakionyeshana kazi katika ardhi ya Urusi, ambao wameweka historia ya kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuwa na presha kubwa ni makocha wa timu shiriki ambao watakuwa na kibarua kizito kwa kuhakikisha wanatwaa taji hilo ambalo hivi sasa linashikiliwa na Ujerumani.

Ifuatayo ni orodha ya makocha 10 wanaovuna mkwanja mrefu ambao wanatarajiwa kutupiwa macho nchini Urusi.

Joachim Low

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Ujerumani, ambaye ndiye anashikilia taji hilo alilolitwaa nchini Brazil kwa kuifunga Argentina bao 1-0.

Huyu ndiye kinara katika orodha ya makocha wanaoingiza mkwanja mrefu akijikusanyia kiasi cha Euro milioni 3.85 ambazo ni sawa na Sh bilioni 10.8 za Kitanzania kwa mwaka.

Tite

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Brazil, anashika nafasi ya pili katika orodha ya makocha wanaovuna mkwanja mrefu kwa makocha watakaoonyeshana kazi Urusi kuanzia Juni 14.

Mkufunzi huyo anachukuwa kiasi cha Euro milioni 3.50 ambazo ni sawa na Sh bilioni 9.8 za Kitanzania kwa mwaka.

Didier Deschamps

Nyota wa zamani wa Ufaransa ambaye alistaafu kucheza soka mwaka 2001, amepewa dhamana ya kuliongoza Taifa hilo nchini Urusi, hizi zikiwa fainali za pili mfululizo kukiongoza kikosi hicho.

Anashika nafasi ya tatu katika orodha ya makocha wanaovuna mkwanja wa Euro milioni 3.5 ambazo ni sawa na Sh bilioni 9.7 za Kitanzania, atakuwa na kibarua kizito nchini Urusi kuthibitisha ubora wake.

Julen Lopetegui

Mlinda mlango wa zamani wa timu ya Taifa ya Hispania, ambaye amekabidhiwa kijiti cha kuwaongoza ‘La Furia Roja’, anashika nafasi ya nne katika orodha ya makocha wanaovuta mkwanja mrefu akiweka kapuni kiasi cha Euro milioni 3 sawa na Sh bilioni 8.4 za Kitanzania.

Stanislav Cherchesov

Aliyekuwa kipa wa kutumainiwa wa Taifa la Urusi, amepewa dhamana ya kukiongoza kikosi cha waandaaji wa fainali hizo, anashika nafasi ya tano katika orodha ya makocha wanaovuna mkwanja mrefu akivuna kiasi cha Euro milioni 2.6 ambazo ni sawa na Sh bilioni 7.3 kwa mwaka.

Fernando Santos

Beki kisiki wa zamani wa Ureno, ambaye amecheza jumla ya michezo 161 akiwa na jezi ya Taifa hilo, alianza kazi ya ukocha mwaka 2010 amekabidhiwa bendera kuhakikisha anarudi na taji nyumbani.

Kocha huyo anakunja kiasi cha Euro milioni 2.25 ambazo ni sawa na Sh bilioni 6.3 za Kitanzania kwa mwaka mmoja.

Carlos Queiroz

Kocha mkuu wa kikosi cha Irani, ambaye pia aliwahi kufanya kazi na mkongwe, Sir Alex Ferguson, katika kikosi cha Manchester United, anashika nafasi ya saba katika orodha ya makocha wanaovuna mkwanja mrefu akichukuwa kiasi cha Euro milioni 2 sawa na Sh bilioni 5.6 za Kitanzania kwa mwaka.

Gareth Southgate

Kiungo wa zamani wa England, ambaye amepewa dhamana ya kuwaongoza ‘Three Lion’ katika ardhi ya Urusi anashika nafasi ya nane katika orodha ya makocha wanaovuna mkwanja mrefu akichukua kiasi cha Euro milioni 2 sawa na Sh bilioni 5.6 za Kitanzania kwa mwaka.

Jorge Sampaoli

Kocha wa zamani wa Chile na klabu ya Sevilla, amekuwa akisifika kwa kufundisha soka lake la kushambulia hivi sasa anaiongoza timu ya Taifa ya Argentina ambayo mwezi uliopita ilikumbana na kichapo cha mabao 6-0 kutoka kwa Hispania.

Mkali huyo anavuna kiasi cha Euro milioni 1.8 ambazo ni sawa na Sh bilioni 5 za Kitanzania kwa mwaka.

Oscar Tabarez

Beki wa zamani wa Uruguay ambalo ndilo Taifa la kwanza kutwaa taji la Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, hii inakuwa mara ya tatu mfululizo kuiongoza timu hiyo katika michuano hiyo mikubwa kuanzia mwaka 2010.

Ndiye anafunga orodha ya makocha wanaovuta mkwanja mrefu ambao wanatarajia kuonyeshana umwamba nchini Urusi, akijikusanyia kiasi cha Euro milioni 1.7 ambazo ni sawa na Sh bilioni 4.8 za Kitanzania kwa mwaka.

@@@@@@@@@@@@@@@

Neymar: Baada ya mwezi nitakuwa fiti

RIO, Brazil

NYOTA wa timu ya Taifa ya Brazil, Neymar Jr, amesema anahitaji mwezi mmoja zaidi ili arudi kwenye hali yake ya kawaida na kuitumikia timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia.

Neymar alifanyiwa upasuaji mwezi uliopita baada ya kupata jeraha katika klabu yake ya PSG, nchini Ufaransa. Hivi karibuni alionyesha video yake mtandaoni akiwa na daktari wake.

“Nahitaji mwezi mmoja ili nirudi katika hali ya kawaida, kwa sasa naendelea vizuri. Kila kitu kinaenda sawa,” alisema Neymar alipofanya mahojiano na Globo TV, Brazil.

Wiki iliyopita Kocha wa PSG, Unai Emery, alisema anaamini nyota huyo ataweza kurejea katika michezo ya mwisho ya Ligue 1.

“Maendeleo yake si mabaya, naamini atarejea mapema hasa michezo ya mwisho ya Ligi Kuu,” alisema Emery.

Ibrahimovic: Nipo tayari kwenda Urusi

STOCKHOLM, Sweden

STRAIKA wa zamani wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic, ameandika kupitia mitandao yake ya kijamii kuwa yupo tayari kucheza fainali za Kombe la Dunia, nchini Urusi.

Ibrahimovic alistaafu kucheza timu ya Taifa ya Sweden mwaka 2016, baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro iliyofanyika nchini Ufaransa.

Lakini baada ya kujiunga na LA Galaxy ya Marekani, amekuwa kwenye kiwango kizuri na kurudisha matumaini kwa mashabiki wake kuwa atarudi tena kuichezesha Sweden.

Ibrahimovic aliandika: “Ninayo nafasi ya kurudi tena Sweden, tutaonana Urusi.”

Nyota huyo anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Sweden, amefunga mabao 62 katika michezo 116.

Demba Ba nafasi anayo Senegal

DAKAR, Senegal

KOCHA wa timu ya Taifa ya Senegal, Aliou Cisse, amesema yupo tayari kumjumuisha mshambuliaji wa Goztepe, Demba Ba, katika kikosi chake kitakachokwenda nchini Urusi.

Ba hajaichezea timu hiyo tangu mwaka 2015, ilitarajiwa angeitwa katika michezo miwili ya kirafiki iliyofanyika hivi karibuni.

Cisse amesema milango iko wazi kwa mshambuliaji huyo aliyefunga mabao matano katika michezo tisa ya klabu yake ya Goztepe.

“Niliwahi kusema, nitaendelea tena kusema kuwa milango iko wazi kwa Demba Ba na wengine.

“Hivi sasa tuna timu iliyokaa zaidi ya miaka mitatu, najivunia kuwa nao,” alisema Cisse.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*