MAJERAHA YAMHARIBIA ‘FUNDI’ MPYA PALACE

LONDON, England


KIUNGO mpya wa Kijerumani aliyesaini Crystal Palace, Max Meyer, huenda asiitumikie timu yake hiyo katika mechi za kwanza msimu wa Ligi Kuu England 2018-19.

Meyer alisaini Palace wiki iliyopita lakini bado yupo kwenye hatua za awali za mazoezi ya kujiandaa na msimu na hayupo tayari kucheza dhidi ya Fulham kesho.

Kabla ya kusajiliwa na timu hiyo, Meyer alikuwa ni mchezaji huru baada ya kuondoka Schalke 04 mwishoni mwa msimu uliopita.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, alianza kujifua kwa mara ya kwanza na wachezaji wenzake wapya Ijumaa iliyopita lakini hakuwemo kwenye mechi yao ya kirafiki dhidi ya Toulouse, iliyochezwa Jumamosi iliyopita, akiwa bado anasaka utimamu wa mwili.

Naye mchezaji mwingine mpya wa Palace, Cheikhou Kouyate, anakabiliwa na dalili ya kutoanza mechi za awali baada ya kukubali kujiunga na timu hiyo akitokea West Ham kwa dau la pauni milioni 10.

Kiungo huyo, Kouyate, alikiri wiki iliyopita kwamba hajui kama atakuwa tayari kucheza dhidi ya Fulham baada ya kupewa mapumziko marefu tangu alipoiongoza timu yake ya taifa ya Senegal katika fainali za Kombe la Dunia.

Kouyate alicheza dakika 17 dhidi ya Toulouse akitokea benchi na ana matumaini ya kuungana na wenzake kwenye mtanange wa ligi dhidi ya Fulham wikiendi hii, ingawa kuna dalili kuwa huenda asicheze mechi hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*