MAJEMBE…. Vifaa hivi lazima vimfuate Zidane Madrid

MADRID, Hispania

 IKIWA ni takribani miezi tisa tangu aondoke katika klabu ya Real Madrid, hatimaye juzi Kocha Zinedine Zidane, amerejea bila kutarajiwa na klabu hiyo ilithibitisha jambo hilo kupitia katika tovuti yake.

Katika kipindi  cha kwanza Zidane  alichokuwa Los Blancos, ilishuhudiwa akifanya makubwa baada ya Mfaransa huyo kuiwezesha kutwaa kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, moja la  La Liga moja la  Supercopa de Espana, mawili ya  UEFA Super Cups na moja la ubingwa wa dunia kwa klabu.

Hata hivyo, tangu alipoondoka Mei mwaka jana na nafasi yake ikachukuliwa na Julen Lopetegui, Real Madrid haikuweza kufanya vizuri na Desemba mwaka huo huo akatimuliwa.

Baada ya kufukuzwa kocha huyo nafasi yake ikachukuliwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Santiago Solari na uteuzi huo ukaonekana kuwa na manufaa katika kipindi cha mwanzo, lakini baadaye Los Blancos ikaanza kusuasua  na kujikuta ikiambulia vipigo viwili  katika mechi ya El Classicos dhidi ya Barcelona kabla ya kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na timu ya Ajax.

Kufuatia hali hiyo ikailazimu Los Blancos kumrejesha Zinedine Zidane ambaye sasa anajukumu la kurejesha imani kwa mashabiki na kuifanya tena  Real Madrid kurejea kwenye ubora wake na kuna wachezaji ambao pengine atahitaji kuwasajili wakati wa dirisha la usajili litakapofunguliwa majira haya ya joto.

Katika makala haya tutaangalia wachezaji watano ambao Zidane anaweza kuwafukuzia katika dirisha hilo la usajili.

 5 Matthjis De Ligt

Nyota huyo wa timu ya Ajax, Matthjis De Ligt, kwa sasa ni mmoja kati ya mabeki bora wa kati duniani na ndiye kwa sasa anashikilia tuzo ya dhahabu  katika nafasi hiyo.

De Ligt hakujaaliwa uwezo wa kuwa beki mahiri tu, bali pia ni mtaalamu wa kupiga pasi na nguvu kimwili na staa huyo ndiye aliyekuwa msaada mkubwa katika ushindi wa Ajax wa mabao 4-1 dhidi ya Real Madrid siku chache zilizopita na kama Los Blancos watampata, anaweza kuwa msaada mkubwa kwao.

Hata hivyo, vigogo hao wanaweza kukumbana na ushindani wa bei kutoka kwa mahasimu wao Barcelona ambao nao wanaonekana kumtaka.

 4. Marcus Rashford

 Marcus Rashford amekuwa akiwindwa mara kadhaa na kikosi hicho cha Los Blancos na pengine Zidane katika usajili wake anaweza kutaka kuwahusisha vijana wenye kipaji kama cha kwake.

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Manchester United imekuwa katika kipindi cha mpito kwa mabadiliko ya makocha na baada ya kutua Ole Gunnar Solksjaer, Rashford ameweza kuimarika zaidi na sasa anajiandaa kuwa mmoja kati ya washambuliaji mahiri duniani.

Hata hivyo, pamoja na uwezekano wa kumpata kuwa ni finyu, lakini kwa uwezo wa Zidane usajili huo unaweza ukafanikiwa.

3 Luka Jovic

 Kwa sasa Luka Jovic ameshadhihirisha uwezo wake mkubwa wa kucheka na nyavu na kiwango alichokionesha katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, kimekuwa ni msaada mkubwa kwa timu yake ya Eintracht Frankfurt.

Msimu huu staa huyo mwenye umri wa miaka 21, ameshasaidia kupatikana mabao 26 ambayo vinara hao wa Ligi ya  Bundesliga wameshayafunga katika mashindano yote.

Akiwa na umri wa miaka 21, staa huyo bado ana muda wa kuimarika zaidi.

 Kwa sasa nyota huyo anawindwa na  Barcelona na huku Real Madrid wakihusishwa kumfukuzia straika huyo.

2. Harry Kane

 Unapozungumzia mastraika mahiri jina la  Harry Kane haliwezi kukosekana.

Hii ni kutokana na kwamba katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na mpaka sasa, nyota huyo wa timu ya Taifa ya England amekuwa kati ya wakali wa kucheka na nyavu duniani.

Msimu huu Kane tayari ameshafunga mabao 17 katika mechi za Ligi Kuu England na bado anazidi kuonesha jinsi alivyo tishio anapokuwa mbele ya lango.

Kama atasajili Kane pengine anaweza kuwa suluhisho la tatizo la ushambuliaji katika safu ya kati ya Los Blancos na suala la Spurs kukosa ubingwa, linaweza kumlazimisha kutua kwenye klabu hiyo ya mji mkuu wa Hispania.

 1. Kylian Mbappe

 Kutokana na kuwa kwa sasa ni kati ya wachezaji chipukizi waliojaaliwa kipaji cha hali ya juu katika soka, haitashangaza jina la Kylian Mbappe kuwamo kwenye orodha ya wachezaji ambao atawataka Zidane apige nao mzigo katika timu hiyo ya Real Madrid.

Ikumbukwe kwamba Zidane alishataka kumsajili Mbappe mwaka 2017 wakati akikipiga katika timu ya AS Monaco, lakini akazidiwa maarifa na klabu ya Paris Saint-Germain.

Naye akiwa na umri wa miaka 20, pengine Zinedine Zidane anaweza kuhakikisha anamchukua ili aweze kuongeza kasi na upatikanaji mabao kwenye safu yake ya ushambuliaji.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*