MAJEMBE MAWILI KUTUA SIMBA

NA ZAITUNI KIBWANA


SIMBA wanatarajia kusajili wachezaji wawili katika dirisha dogo la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, linalotarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu.

Kamati ya usajili ya Simba inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Zakaria Hanspope, inaendelea kufanya usajili kwa umakini baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, kupendekeza idara ambazo anahitaji kuongozewa nguvu.

Inasemekana Omog raia wa Cameroon, anahitaji kuongeza nguvu idara ya ushambuliaji licha ya mzunguko wa kwanza kuwasajili Laudit Mavugo kutoka Burundi na raia wa Ivory Coast, Fredrick Blagnoon na pia kupata kipa mwingine mzoefu.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu wa Kamati ya Usajili Simba, Kassim Dewji, alisema wanatarajia kusajili wachezaji wawili wapya kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Dewji ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba, alisema wanaendelea kufanya usajili kwa umakini ikiwemo pia kupata kipa atakayesaidiana na Vincent Angban, Manyika Peter Jrn na Denis Richard.

Alisema katika ripoti ya benchi la ufundi hawakupendekeza wachezaji wao kuachwa, kwani hawajaona upungufu wao baada ya kucheza mechi 15 za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

“Tuna nafasi mbili tu ambazo tutafanyia usajili na hii inatokana na mapendekezo ya benchi letu la ufundi,” alisema Dewji.

Dewji alisema katika kuhakikisha wanatimiza matakwa ya benchi la ufundi, wameanza kufanya mazungumzo na kipa wa African Lyon raia wa Cameroon, Youthe Rostand.

Alisema wanatarajia kumalizana na kipa huyo wiki ijayo baada ya kuridhishwa na uwezo wake wa kudaka, huku wakiendelea kumtafuta mshambuliaji.

Katika hatua nyingine, Dewji alisema kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Awadh Juma, ataendelea kuitumikia timu hiyo, licha ya  Kagera Sugar kumhitaji.

“Sisi tumesema hakuna mchezaji  atakayeachwa sasa, hao wanaotaka wachezaji wetu, hakuna atakayeondoka hapa,” alisema.

Kauli ya Dewji pia inaonekana kuzima ndoto za mchezaji, Abdi Banda ambaye tayari ameaga ndani ya kikosi hicho, akisema ni wakati mwafaka sasa wa yeye kuondoka.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*