MADOLA ZIMEBAKI SIKU 90, MAANDALIZI BADO CHANGAMOTO

NA WINFRIDA MTOI

KIFIMBO cha Malkia wa Uingereza, kiliwasili nchini Aprili mwaka jana, kuashiria kuanza maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola yanayotarajia kufanyika Aprili mwaka huu, katika Mji wa Gold Coast, Australia.

Ni utaratibu wa kawaida inapokaribia michezo hiyo kukimbiza kifimbo cha Malkia kwa nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Madola  kwa kuwakutanisha wadau wa michezo.

Kifimbo hicho kilipowasili nchini tulishuhudia viongozi mbalimbali wa michezo na wanamichezo wakiwa katika msafara wa mapokezi na kukikimbiza maeneo maalumu yaliyopangwa kupita jijini Dar es Salaam.

Suala kubwa linalozungumziwa katika mapokezi ya kifimbo cha Malkia ni  kuhusu maandalizi ya timu zinazotarajia kwenda kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola.

Lakini pia shuhuda zilizotolewa na wanamichezo waliowahi kufanya vizuri katika michezo hiyo.

Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ndiyo yenye jukumu la kuteua na  kusimamia vyama kuhakikisha vinapeleka wanamichezo bora katika michezo hiyo.

Tayari OC imeonekana imefanya kazi  katika sehemu yake kwa kufanikiwa kuteua vyama vitano vitakavyotoa wanamichezowatakaokwenda  Australia kushiriki Madola.

Wanamichezo watakaoiwakilisha nchi  katika michezo ya mwaka huu ni ngumi, riadha, meza, kuogelea na paralimpiki, ingawa maandalizi yao hayajawatia moyo Watanzania kwa wao kuweza kurejea na medali.

Kama ilivyo, TOC wamekuwa wakisisitiza juu ya kufanya maandalizi bora, baada ya kifimbo cha Malkia kuwasili, lakini kinachoonekana mambo bado hayako sawa, ukizingatia zimebaki siku 90 kabla ya kuanza kwa michezo ya Jumuiya ya Madola.

Binafsi naweza kusema kuna changamoto ya maandalizi kwani mpaka sasa haijafahamika wanamichezo wangapi wamefikia viwango vya ubora vinavyohitajika ili kushiriki michezo kwa ufanisi mkubwa.

Changamoto ya kwanza iliyopo  kwa wanamichezo wanaotarajiwa kwenda kushiriki michezo hiyo ni kambi za pamoja.

Ukiangalia katika michezo yote mitano itakayoiwakilisha nchi katika Madola  suala la kambi limekuwa ni ishu kubwa, kwani wachezaji wanafanya mazoezi yale ya kawaida  yaliyozoeleka, ambayo hayaendani na ushindani wa kimataifa.

Mfano mzuri timu ya ngumi za ridhaa, imeanza mazoezi muda mrefu pale viwanja vya wazi vya Uwanja wa Taifa wa Ndani jijini Dar es Salaam, lakini  haionyeshi itakwenda kushindana katika michezo ya Jumuiya ya Madola.

Haiwezekani timu inajiandaa  kushiriki mashindano makubwa kama Jumuiya ya Madola halafu inafanya mazoezi bila vifaa muhimu, lakini wachezaji wakitoka nyumbani kwenda kufanya mazoezi.

Awali ilitangazwa kuwa timu ya ngumi ingekwenda kuweka kambi nchini Cuba kwa zaidi ya miezi sita kujiandaa na michezo ya Madola, lakini mpaka sasa mabondia hao wanaendelea kufanya mazoezi katika viwanja vya mchangani.

Tumeona nguvu walizoanza nazo chama cha riadha na kuogelea, kujiandaa na  michezo hiyo zinazidi kupungua, kwani hakuna chama kilichoonyesha nia ya  kuwaweka wachezaji katika kambi ya pamoja.

Septemba mwaka jana, riadha walitangaza kuweka kambi ya muda mrefu wilayani Lushoto, mkoani Tanga ambayo ilipangwa kuanza Novemba mwaka jana mpaka Aprili  mwaka huu, lakini hakuna lililofanyika.

Kwa upande wa kuogelea tayari wameweka wazi majina ya wachezaji wanne watakaokwenda kushiriki michezo hiyo, lakini mpaka sasa hakuna kambi ya pamoja ya wachezaji, kila mchezaji anafanya mazoezi binafsi.

Wachezaji waliochaguliwa na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) ni Hilal Hilal anayejifua Dubai, Collins Saliboko na Sonia Tumiotto, Celina Itatiro yupo  Dar es Salaam akifanya mazoezi kwenye Klabu ya Dar Swim.

Mpira wa meza waliokuwa wanasuasua muda wote kuanza maandalizi, wenyewe  wamekwenda kuweka kambi nchini China ambako watapata michezo ya kufuzu viwango huku paralimpiki wakiendelea na mazoezi lakini changamoto waliyokuwa nayo ni kama ya wenzao wa ngumi.

Kutokana na hali inayoendelea katika maandalizi kama jitihada za dhati hazitachukuliwa kuhakikisha wanamichezo hao wote wanapata kambi za pamoja, kuna uwezekano mkubwa Tanzania ikatia aibu Australia.

Ifahamike kuwa wanamichezo wanaokwenda kushiriki michezo hiyo watakutana na upinzani mkali kutoka kwa mataifa makubwa duniani yaliyojiandaa vizuri kushindana, hivyo kukosekana na maandalizi bora kunaweza kuwafanya kurejea mikono mitupu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*