googleAds

Macho yote kwa Samatta England leo

Birmingham, England

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Aston Villa, Mbwana Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo anaweza kuwa kwenye kikosi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City.

Kama atapata nafasi hiyo, basi utakuwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea K.R.C Genk ya nchini Ubelgiji kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 10 ambazo ni zaidi ya bilioni 29 za Kitanzania.

Mchezo huo ni nusu fainali ya pili ya Kombe la Ligi, ambapo mchezo wa kwanza Leicester City wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani walilazimishwa sare ya bao 1-1, hivyo leo lazima apatikane mshindi kwa ajili ya hatua inayofuata.

Samatta alijiunga rasmi na klabu hiyo ya Aston Villa, Jumatatu ya wiki iliyopita na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kujiunga na klabu inayoshiriki Ligi Kuu England.

Kocha mkuu wa timu hiyo ya Aston Villa aliweka wazi kuwa Samatta alijiunga na wachezaji wenzake kwenye mazoezi ya pamoja tangu wiki iliopita, hivyo amefurahishwa na kiwango chake alichokionesha.

“Samatta amefanya mazoezi na wachezaji wenzake, ameonesha kuna kitu anacho, hivyo sina wasiwasi naye, ninaamini atakuwa na mchango mkubwa kwenye timu, siwezi kusema atakuwa kwenye kikosi cha kwanza au atatokea benchi, ila ni wazi Samatta yupo fipi kwa ajili ya kucheza,” alisema kocha huyo.

Samatta ana kila sababu ya kuwa kwenye kikosi hicho cha kwanza kwa kuwa timu hiyo haina mshambuliaji mkubwa zaidi yake, hivyo kuna uwezekano huo wa kusimamishwa namba tisha na kuipigania timu.

Aston Villa kwenye msimamo wa Ligi inashika nafasi ya 16, ikiwa na jumla ya pointi 25 baada ya kucheza michezo 24, hivyo wanaamini wana nafasi kubwa ya kubaki kwenye ligi msimu ujao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*