LWANDAMINA: YANGA WATANIKUMBUKA

NA HUSSEIN OMAR

SIKU chache baada ya kocha wa Yanga, George Lwandamina, kujiunga na klabu yake ya zamani ya Zesco amefunguka kwamba ipo siku viongozi wa Wanajangwani hao watafunga safari kwenda Zambia kumpigia magoti ili arejee kuifundisha timu hiyo.

Kocha huyo anayejulikana kwa jina la utani la ‘Chicken Man’ nyumbani kwao Zambia, alikuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Zesco United kabla ya juzi kufanya uamuzi mgumu wa kurejea klabu yake hiyo ya zamani.

Akizungumza na BINGWA juzi, Lwandamina alisema yeye ni mmoja kati ya makocha bora waliowahi kutokea katika Ukanda wa Bara la Afrika, hivyo kurejea kwake Zesco kunatokana na mabosi wa timu hiyo kutambua uwezo wake.

“Mimi ni mmoja wa kati ya makocha 10 bora wa Kiafrika, ndio maana sikubabaishwa na siasa za soka la Tanzania kwa kuwa  nilijua naweza kuondoka muda wowote,” alisema Lwandamina.

“Najua ipo siku watakuja viongozi wanaojua mpira na kuthamini taaluma ya makocha, watakuja kunifuata na kunipigia magoti nirejee kuifundisha Yanga kwa sababu sikuondoka kwa ubaya,” alisisitiza Lwandamina.

Alisema anasikitika kuondoka Yanga, huku akiwa ameifundisha timu hiyo asilimia 40 ya ujuzi wake kutokana na kutumia muda wake mwingi kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kuwafundisha namna ya kuishi nje ya uwanja.

“Nasikitika sijatumika ipasavyo, lakini kama nilivyokwambia, nasisitiza tena, ipo siku wanaotambua uwezo na thamani yangu watakuja tena kunifuata nirejee kuifundisha Yanga, “ alisisitiza Lwandamina.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*