LWANDAMINA AONYESHA VITU ADIMU YANGA

NA HUSSEIN OMAR

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, ameendelea kuonyesha vitu adimu kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana jioni kwenye Uwanja wa Gymkhana uliopo Posta jijini Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo, Lwandamina alionyesha kuwa si mtu wa mchezo mchezo kutokana na kutoa vitu vya kipekee kwa nyota wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Akionekana amepania kutengeneza kikosi cha kucheza kwenye hali yoyote, Lwandamina aliwaingiza wachezaji wa Yanga uwanjani kwa ajili ya kuanza mazoezi majira ya saa 8:30 mchana wa jua kali.

BINGWA lilishuhudia benchi zima la ufundi la Yanga likiongozwa na George Lwandamina na msaidizi wake, Juma Mwambusi, likianza ‘programu’ yao ya siku kwa kuwapa mazoezi mepesi wachezaji wa timu hiyo.

Mara baada ya kumaliza mazoezi mepesi, Lwandamina aligawa timu kwenye makundi matatu na kuanza kuuchezea mpira na kuwapa mbinu za kufanya mashambulizi ya kushtukiza (Counter Attack), zoezi ambalo lilifanywa vyema na nyota wa timu hiyo.

Katika zoezi hilo, nyota wa Yanga walionekana kuimarika zaidi kutokana na kupiga pasi za haraka na uhakika, lakini pia katika suala zima la ukabaji ambapo kila mmoja alikuwa makini kwenye kukaba.

Zoezi hilo lilidumu kwa zaidi ya dakika 45 ambapo BINGWA lilishuhudia mshambuliaji wa timu hiyo, Malimi Busungu ambaye alikuwa nje ya uwanja muda mrefu, akirudi kwa kasi ya ajabu kwenye mazoezi hayo.

Mbali na Busungu, mchezaji mwingine aliyeonyesha vitu adimu kwenye mazoezi hayo, ni kipa Beno Kakolanya ambaye aliokoa michomo mingi langoni lakini moja kati ya vitu adimu alivyovifanya kipa huyo, ni namna alivyoweza kudaka mipira pale washambuliaji wa timu hiyo, Donald Ngoma na Malimi Busungu walipobaki naye.

Baada ya kumaliza zoezi, Lwandamina aligawa vikosi viwili; kikosi cha kwanza na cha kile cha pili na kuanza kucheza mechi mazoezi ambapo katika zoezi hilo,  kiungo Said Juma Makapu alionekana kupangwa katika kikosi cha kwanza na kufanya kweli.

Kikosi cha kwanza kilikuwa hivi: Deogratius Munish Dida, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Andrew Vincent, Makapu, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya na Donald Ngoma.

Kikosi cha pili: Ali Mustapha ‘Barthez’, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Mbuyu Twite, Thaban Kamusoko, Malimi Busungu, Anthony Matheo na wengine.

Katika hatua nyingine, jana baada ya mazoezi, benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na Lwandamina, lilimweka kitimoto straika wa timu hiyo, Malimi Busungu, kutokana na kukutwa na majanga kadhaa ya nje ya uwanja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*