LWANDAMINA AANZA KAZI ZESCO

*Jese Were, wenzake kicheko

*Kurejea Jangwani kuanika kila kitu

ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR

KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ameanza rasmi kibarua chake kipya na klabu yake ya zamani ya Zesco United, baada ya kuachana na Wanajangwani.

Lwandamina ambaye aliwasili Zambia juzi, ameanza kibarua chake rasmi jana baada ya kutambulishwa kuchukua nafasi ya Tenant Chembo, anayekwenda kuinoa timu tajiri ya Buildcon iliyopanda ligi.

Kwenye utambulisho huo, wachezaji wa Zesco wakiongozwa na Jese Were, walionekana kufurahishwa na ujio wa kocha huyo mzawa aliyeipa mafanikio makubwa timu hiyo wakati akiifundisha.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Lwandamina alijumuika pamoja na wachezaji wa timu hiyo na kuanza rasmi kibarua chake hicho.

Katibu Mkuu wa Zesco United, Richard Mulenga, alithibitisha na kusema kuwa Lwandamina ametambulishwa mara mbili toka amefika nchini Zambia.

Mulenga alisema mara baada ya utambulisho huo, Lwandamina atarejea Dar es Salaam na ataanza majukumu mapya mwishoni mwa mwezi ujao wakati mkataba wake na Yanga utakapokuwa umemalizika.

Hata hivyo, Lwandamina leo (jana) alitarajiwa kuwepo jukwaani kushuhudia Zesco United ikiikabili Lusaka Dyanamos katika mchezo wa Ligi Kuu Zambia.

Lwandamina alikuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Zesco United, kwani aliiongoza Zesco kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zambia na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia maarufu Chipolopolo, alidaiwa kusaini mkataba wa awali na kikosi hicho na kilichobakia ni kumalizana tu na walitarajia kufanya hivyo mwishoni mwa mwezi ujao ambao ndiyo kocha huyo anamaliza mkataba wake na Yanga.

Kwa upande wao, wachezaji wa timu    hiyo walionekana kufurahishwa na ujio wa kocha huyo, huku wakimmwagia sifa kedekede kwa kusema kuwa ni mmoja wa makocha bora Afrika.

Straika wa timu hiyo ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini humo, Jesse Were, alisema ni kocha aliyewahi kufanya naye kazi hivyo ujio wake Zesco utawapa matumaini ya kufanya vema zaidi.

“Nimewahi kufanya naye kazi, ni kocha mzuri ujio wake wa mara ya pili utatusaidia kutetea ubingwa wetu msimu huu,”  alisema.

Naye Fackson Kapumbu, alisema “George ni kocha mshindi, kila anapoenda hufanya vizuri. Anatengeneza hali ya kujiamini na kupambana kwa wachezaji kuanzia ndani na nje ya uwanja. Ni kocha wa kiwango cha juu sana.”

Katika hatua nyingine, kocha huyo anatarajia kurejea nchini wakati wowote kuanzia sasa kumalizia mkataba wake na kuwaaga wachezaji wa Yanga.

Kwa sasa Yanga inanolewa na makocha wasaidizi, Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa wakiwa na kocha wa makipa, Juma Pondamali.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*