Lulu: Hakuna ninachojutia kwenye maisha yangu

NA MWANDISHI WETU

MWIGIZAJI nyota nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, amesema hakuna jambo  lolote analojutia kwenye maisha yake kwa kuwa yamemjenga na kuwa imara kama alivyo sasa.

Akizungumza jana na kipindi cha XXL ya Clouds Fm, Lulu alisema anaamini katika mambo mazuri na mabaya aliyoyafanya yamekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yake ya sasa.

“Kiukweli hakuna ninachojutia kwenye maisha yangu, sababu naamini katika kila zuri na baya nililolifanya limefanya niwe hivi nilivyo, pengine nisingefanya miaka mitano iliyopita, ningefanya leo wakati ndiyo naelekea kuwa mtu mzima.

“Ingekuwa kichekesho zaidi na sijutii kwa sababu kwenye kujutia kuna kujilaumu na kujihukumu,” alisema Lulu.

Kelly Haso awachana wanaotelekeza watoto

NA MWANDISHI WETU

MSANII wa kizazi kipya kutoka bendi ya Bogoss Musica, Ally Said ‘Kelly Haso’, amesema vitendo vya wanawake kutelekeza watoto vinapaswa kukemewa vikali na jamii wakiwamo wasanii.

Akizungumza na Papaso la Burudani, Kelly Haso alisema ndiyo maana ameamua kuachia wimbo wa Come Back ambao maudhui yake yamelenga kumrudisha mama kwa mtoto wake.

“Nachukia hiyo tabia, wazo la wimbo huo alinipa mama yangu nikaamua kurekodi na nashukuru mapokezi yamekuwa makubwa kwa sababu haya matatizo yapo mengi kwenye jamii,” alisema Kelly.

Jana historia yazinduliwa Mtwara

NA BRIGHER MASAKI

MWIMBAJI wa nyimbo za Injili kutoka Mtwara, Meshack Kapula, ameweka wazi kuwa wapenzi wa muziki huo wajiandae kuipokea albamu ya Jana Historia itakayozinduliwa Mei 5, mwaka huu mkoani humo.

Akizungumza na Papaso la Burudani jana, Meshack alisema albamu hiyo ina jumla ya nyimbo sita na itakuwa katika mfumo wa audio, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi siku hiyo.

“Kila kitu kipo sawa, uzinduzi utafanyika katika Kanisa la KKKT Mnarani kuanzia saa tisa mpaka saa 12 jioni, pia nitasindikizwa na The Voice kutoka Dar es Salaam, The Heaven Voice na Miss Agatha,” alisema Meshack.

Uzalendo Kwanza wapata dili la ubalozi

NA JEREMIA ERENEST

WASANII wanaounda umoja wa Uzalendo Kwanza, wamepata dili la ubalozi wa kutangaza utalii wa ndani katika mbuga za Biharamulo, Burigi na Kisini ‘BBK’ zilizopo Mkoa wa Kagera.

Steve Nyerere ambaye ni Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, alisema hiyo imekuwa bahati kwao na watatenda haki kwa kutembelea mbuga hizo pamoja na Chato ambako kuna vivutio vingi vya utalii.

 “Utalii ni sekta muhimu hapa nchini, tumepewa kazi ya kutangaza mbuga hizi, tutafanya kazi hii kwa moyo kwa kuwa tunajua mapato ya utalii ndiyo yanatumika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisema Nyerere.

Naye Balozi wa Utalii, Nangasu Warema, alisema mbuga hizo ni mpya hivyo zitakuwa zinatangazwa na chama cha utalii, pia wataongeza mabalozi wengine kutoka sekta mbalimbali.

Msando kuupitia mkataba wa Wema Sepetu

NA JEREMIA ERNEST

MWANASHERIA wa mwigizaji Wema Sepetu, Albert Msando, ameshangazwa na picha za mrembo huyo akisaini mkataba ambao yeye haujui hivi karibuni na kampuni moja ya ving’amuzi.

Akizungumza katika kongamamo la waigizaji lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Msando alisema anashangazwa na mteja wake anasaini mkataba bila yeye kufahamu.

“Nilishangaa kuona picha kwenye mtandao Wema  anasaini mkataba wakati hajanifahamisha wala sijui chochote, sasa naomba Wema ulete huo mkataba ili niupitie,” alisema Msando.

Aliongeza kuwa wasanii wanatakiwa kuwa makini katika mikataba wanayoingia kwa kushirikisha wanasheria.

Drake adaiwa kuwapa mkosi wachezaji

ROMA, ITALIA

RAPA bora zaidi kwa sasa duniani, Aubrey Drake, ametuhumiwa kuwapa mkosi wachezaji wa soka mara baada ya kupiga nao picha na timu zao kufungwa pindi zinapocheza.

Juzi klabu ya As Roma ya nchini Italia iliwaonya wachezaji wake kupitia ukurasa wao wa Twitter kutopiga picha na Drake mpaka msimu huu uishe ili kukwepa kufungwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya mashabiki kutoa orodha ya wachezaji waliopiga picha na Drake kisha timu zao zikafungwa kama vile Jadon Sancho wa Dortmund timu yake ikafungwa mabao 5-0 na Tottenham.

Hali kadhalika Aubameyang wa Arsenal ni siku chache mbele timu yake ikafungwa bao 1-0 na Everton pia, Kun Aguero pia wa Man City alipiga picha na Drake na akakosa penalti na timu yake ikafungwa bao 1-0 na Tottenam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*