Lulu Diva, Wakazi hapatoshi Kigamboni mkesha wa Pasaka

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kusherehekea mkesha wa Sikukuu ya Pasaka, mamia ya mashabiki wa Bongo Fleva wanaoishi Kigamboni, Dar es Salaam, wanatarajia kupata burudani ya nguvu kutoka kwa Lulu Diva na rapa Wakazi.

Mratibu wa onyesho hilo, Mbwana Khamis, alisema wasanii hao watadondosha burudani katika klabu ya usiku ya Jembe One kuanzia saa mbili usiku na kuendelea.

“Mbali na Lulu Diva na Wakazi, kutakuwa na burudani ya kutosha kutoka kwa Dj Dully na Dj Slay, hivyo wakati wote wa Kigamboni na maeneo ya jirani waingie kwa uchakavu wa 5,000 tu,” alisema Mbwana.

Eric Kisindja kuachia Siwezi Lipa

NAIROBI, KENYA

BAADA ya kufanya vizuri na wimbo Ayubu aliomshirikisha Natasha Lisimo, mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Nairobi, Kenya, Eric Kisindja, amewaomba mashabiki wa Tanzania kuipokea upya video yake mpya Siwezi Lipa inayotoka kesho.

Akizungumza na Papaso la Burudani, Eric ambaye ni pia ni mhubiri wa neno la Mungu, alisema wimbo Siwezi Lipa ni maalumu kwa ajili ya Pasaka kwa kuwa umebeba ujumbe unaoendana na sikukuu hiyo kubwa duniani.

“Video ninaipokea leo kutoka kwa mwongozaji wangu na kesho itakuwa kwenye chaneli yangu ya YouTube, ndani ya Siwezi Lipa nimeimba nikimwambia Yesu Kristo ya kwamba siwezi lipa gharama na wema aliotenda kwa wanadamu mpaka tumekuwa huru, tumeokolewa kuna gharama alilipa ambayo hakuna mwanadamu anaweza kulipa,” alisema Eric.

Maria Msalilwa atoa moja toka kwenye albamu

NA BRIGHER MASAKI

MWIMBAJI wa nyimbo za Injili nchini, Maria Msalilwa, ameachia video ya kwanza iliyobeba jina la albamu yake ya Barabara ya Mafanikio ikiwa imeongozwa na Epic Films.

Akizungumza na Papaso la Burudani, Maria, alisema albamu hiyo itakuwa na mkusanyiko wa video nzuri zilizobeba jumbe zenye kuinua na kubariki na anaisambaza na yeye mwenyewe ndani na nje ya Dar es Salaam.

“Barabara ya mafanikio ni wimbo uliobeba ujumbe mzuri wa kutukumbusha juu ya safari ya maisha ya mwanadamu kwamba si nyofu bali ni yenye vikwazo na vizingiti vingi hivyo yakupasa kuwa na imani pamoja na uvumilivu ili uweze kufika salama katika vyote tunavyotarajia vifanikiwe,” alisema Maria.@@@

Amigo jukwaa moja na Papii Kocha

NA JEREMIA ERNEST

MFALME wa taarabu nchini, Prince Amigo, amesema ndoto yake ya kufanya kazi na Papii Kocha inakwenda kutimia Aprili 21, mwaka huu katika jukwaa la Cheers Night, katika ukumbi wa Traventine, Magomeni, Dar es Salaam. 

Akizungumza na Papaso la Burudani, Amigo, alisema tangu Papii aachiwe huru alikuwa anatamani siku wafanye onyesho la pamoja.

“Nilikuwa napanga kufanya shoo pamoja na Papii Kocha kwa kuwa nilikuwa shabiki wa nyimbo zake wakati nikiwa bado sijatoka kimuziki, kwa hiyo mashabiki wajitokeze kwa wingi na kiingilio ni 8,000,” alisema Amigo.

@@@

Miss Morogoro yaendelea kukaribisha wadhamini

NA JEREMIA ERNEST

MWANDAAJI wa Miss Morogoro, Farida Fujo, amesema milango ipo wazi kwa kampuni na taasisi zinazotaka kudhamini shindano hilo mwaka huu.

Akizungumza na Papaso la Burudani, Fujo, alisema mbali na kuziomba kampuni na taasisi kujitokeza kudhamini Miss Morogoro, nafasi zipo wazi warembo kuanza kuchukua fomu.

“Nafasi zipo wazi kwa warembo ambao wana vigezo wanaweza kufika Nyumbani Park Hotel, tumejipanga kuboresha shindano hili hadi mrembo wetu atwae taji la Miss Tanzania,” alisema Fujo.

Kanda ya Morogoro ilitoa zawadi ya gari mwaka jana kwa mshindi wa kwanza, Amer Kubri. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*