LUGOLA AWAGEUKIA NYOTA SIMBA

NA MWANDISHI WETU


BAADA ya Simba kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Asante Kotoko ya Ghana katika mchezo wa Tamasha la Simba ‘Simba Day’, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Kange Lugola, amewataka wachezaji wa timu hiyo  kuthamini nembo ya klabu hiyo ili kuleta matokeo chanya.

Mchezo huo ulichezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lugola  aliyasema hayo  katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa maalumu kwa ajili kuwapongeza wachezaji wa Simba na Asante Kotoko iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam juzi.

“Wachezaji wajue thamani ya nembo ya Simba na kila wanachokifanya wajue matokeo yake yatakuwa katika faida ipi kwa timu na klabu yao kwa ujumla.

“Ili kuifurahisha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya JPM (John Pombe Magufuli), basi hakuna budi Simba kukunjua makucha yake na kuonyesha uhalisia wa mnyama Simba kwa vitendo. Tunataka kuona mnyama akiunguruma, si  eti Simba akiona swala anakula,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo  alisisitiza kulivalia njuga suala la utengenezaji wa jezi feki.

Lugola aliwataka viongozi wa Simba kwenda ofisini kwake kwa lengo la kupanga mkakati utakaofanikisha oparesheni maalumu ya kuwanasa kwa urahisi wote wanaohujumu mali zao.

“Viongozi mjipange tufanye operesheni, ninaahidi hawatarudia na suala hilo kuwa historia labda nisiendelee kuwa waziri.

“Ninataka kuona wenye nembo wazalishe peke yao, wajanja wakae mbali kabisa,” aliongeza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*