Low ndiye wa kuulizwa tatizo Ujerumani?

NA HASSAN DAUDI

MIAKA michache tu iliyopita, Ujerumani ilikuwa moja kati ya timu zilizokamilika zaidi kwenye uso wa dunia.

Walifanya kila walichokitaka, na kumbukumbu za wengi zitawapeleka katika Uwanja wa Mineirao kule Brazil, walipowachapa wenyeji wao mabao 7-1.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanaamini timu inapofika katika kilele cha ubora wake, njia rahisi ambayo hubaki ni kuanguka.

Hiyo ndiyo hali wanayoishi nayo Wajerumani kwa sasa. Wanaporomoka kwa kasi katika utawala wao wa kandanda.

Kuanguka kwa Ujerumani hivi sasa kuna mambo mawili ambayo yameizunguka timu hiyo iliyoingia matatizoni na baadhi ya wachezaji wake hivi karibuni.

Mosi, kuna uwezekano mkubwa hivi sasa kila timu imetambua jinsi gani ya kucheza na Ujerumani kimbinu na kiufundi, kwa kiasi kikubwa wapinzani wameonekana kuwamudu mabingwa hao wa zamani wa dunia.

Wapo wanaoamini katika kujilinda, kisha kutumia mipira mirefu kwa wachezaji wao wenye kasi ‘counter attacking’, lakini wengine huamini kwenye kuziba nafasi kwa kutoa presha kubwa kwa viungo wa Ujerumani na kisha kutumia makosa yao kuiadhibu timu hiyo.

Mambo yote hayo yalionekana katika michezo ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Urusi mwaka huu na kupelekea Ujerumani kutolewa hatua ya makundi.

Pili, inawezekana Kocha wa Ujerumani, Joachim Low, anahitaji mbinu mpya ili kuinyanyua timu yake iliyokwama kwenye matope mazito.

Kivipi? Kutokana na wapinzani kutambua jinsi ya kucheza na Ujerumani, Low inabidi akune kichwa kwa mara nyingine kuunda mbinu ambazo zitakuwa mbadala zaidi.

Ujerumani inapiga pasi nyingi inapokuwa mbele ya eneo la hatari la wapinzani wao, labda wanahitajika kurudi katika utamaduni wao wa kupiga mashuti makali kutoka nje ya eneo hilo.

Lakini kwa kiasi kikubwa hata hao akina Toni Kroos wanaonekana kubadilika na kuingia kwenye kile kilichopo hivi sasa kwa kufuata kipi ambacho kocha anakihitaji.

Mbele ya eneo la wapinzani ambalo wanapiga pasi nyingi, Ujerumani imekosa mchezaji mbunifu wa kufanya hilo lionekane zaidi kwa timu hiyo.

Mesut Ozil alikuwa injini wa kila kitu katika timu hiyo pindi suala la ubunifu lilipohitajika. Hivi karibuni Joshua Kimmich amekuwa akitumika kwenye kiungo ili kuifanya timu hiyo kuwa na nguvu, mamlaka zaidi dhidi ya wapinzani wao.

Kimmich si mgeni eneo hilo, lakini hajatumika kwa muda mrefu kama ilivyokuwa pindi anacheza beki wa kulia, anapokutana na viungo asilia wanaojua majukumu yao huwa ngumu kutamba mbele yao.

Upande mwingine, mambo ya akina Ozil ambayo yalitokea na kuigawa timu hiyo inawafanya kuwa kwenye wakati mgumu hivi karibuni.

Low anahitaji kitu kipya kwa ajili ya timu yake au nje ya hapo aamue kukaa pembeni na kuondoka kwa heshima ndani ya timu hiyo ambayo imeweka rekodi ya kufungwa michezo sita katika kalenda ya mwaka huu.

Low yupo katika wakati mgumu, lakini furaha zaidi ni kwa wale waliomwaga machozi yao miaka minne iliyopita katika Uwanja wa Mineirao.

Pepo ya Low imezungukwa na wachezaji wengi wenye uwezo na vipaji, lakini mateso makali kwake pindi wanaposhindwa kupata matokeo kama ilivyokuwa zamani.

Kwa hali inavyozidi kuwa ngumu kwa Ujerumani kila kukicha, Low inabidi aondoke mwenyewe au aondoshwe kwa aibu ya kufukuzwa.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*