Liverpool? Mapema mno kupeleka ubingwa Merseyside

SI jambo linaloshindikana lakini nachelea kusema, tunahitaji muda kidogo kuamini na kuwaaminisha wengine kuwa sherehe za ubingwa zitafanyika mjini Mereseyside, mwishoni mwa msimu huu.

Kutokana na aina ya soka lao la kushambulia, mwenendo wao kwenye ligi, uzoefu wa kocha Jurgen Klopp, ubora wa akina ‘Mo’ Salah, hakuna atakayebisha kuwa Majogoo wana nafasi ya ubingwa walioukosa kwa miaka 28.

Lakini je, haikuwa hivyo msimu wa 2013-2014? Liverpool iliyokuwa na safu kali ya ushambuliaji chini na Luis Suarez, Daniel Sturridge na Raheem Sterling, kocha akiwa ni Brendan Rodgers, haitofautiani sana na hii ya leo.

Kama ilivyo sasa, kufikia hatua hii tayari kule Merseyside kulishaamka kwa shamrashamra za kulisubiri taji la Ligi Kuu. Tayari mashabiki wa Liverpool walishajua ni zamu yao.

Ushindi dhidi ya waliokuwa wapinzani wao wakubwa, Man City, uliwafanya Majogoo wawe kileleni kwa tofauti ya pointi tatu zikiwa zimebaki mechi tano tu kabla ya ligi kumalizika.

Upepo ulibadilika ghafla katika mechi yao ya 34, walipotandikwa na Chelsea, tena nyumbani kabla ya kutoa sare ya mabao 3-3 na Crystal Palace. Mwishowe, sherehe za ubingwa zikahama vichwani mwa mashabiki wa Liverpool waliozishuhudia zikifanyika jijini Manchester.

Ni kwa mazingira hayo basi, ni mapema mno kwa mashabiki wa Liverpool kutamba kuwa tayari taji la Ligi Kuu ni la kwao. Ukikitazama kikosi cha kocha Klopp, tunaweza kukubaliana kuwa haitashangaza endapo ndoto za Liverpool zitaota mbawa kwa mara nyingine.

Wakati ikibanwa mbavu na West Ham katika sare ya bao 1-1, Liverpool iliwakosa nyota wake wanne wa kikosi cha kwanza kutokana na majeraha. Joe Gomez, Trent Alexander-Arnold, Gini Wijnaldum na Jordan Henderson, waliitazama mechi hiyo wakiwa wanauguza majeraha yao.

Ikizingatiwa kuwa bado Liverpool wana mechi zaidi ya 13, unaweza kuona ni kwa kiasi gani inaweza kupoteza dira endapo itakutana na timu ngumu kipindi hiki ambacho nyota hao wanaendelea kuwa nje ya uwanja.

Pia, lipo suala la kisaikolojia kwa wachezaji wa sasa wa Liverpool, ambalo kwa namna moja au nyingine linaweza kuwavuruga na kujikuta wakipishana na ubingwa.

Ikumbukwe kuwa timu hiyo haijachukua ubingwa tangu mwaka 1990. Kwa maana hiyo, matarajio makubwa ya mashabiki wa Liverpool ni kuona kiu yao ikikatwa na kikosi hiki cha Jurgen Klopp. Hiyo inawaongezea presha wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla.

Wakati huo huo, historia inaonesha wazi kuwa timu ambazo hupewa presha kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano fulani, hushindwa kufurukuta kutokana na presha ya wale wanaoziamini.

Ilikuwa hivyo miaka minne iliyopita katika fainali za Kombe la Dunia. Hata kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, sehemu kubwa ya mashabiki wa soka ulimwenguni iliwapa nafasi wenyeji, Brazil.

Si tu kwa kuwa mashindano yalikuwa yakifanyika kwenye ardhi ya nyumbani, mashabiki wa kandanda walivutwa na ubora wa kikosi cha ‘Selecao’. Neymar, David Luis, Dani Alves, Fernandinho, Marcelo, Oscar, Willian, kilikuwa na kila sababu ya kulibeba taji hilo.

Ndani ya nchi, wachezaji wa Brazil walikumbana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wao. Hata wachezaji wenyewe, kila mmoja alitaka kuweka historia ya kulibeba taifa mbele ya baba, mama, dada na ndugu zake wengine.

Ni presha hiyo ndiyo iliyosababisha Brazil wakaishia nusu fainali, tena kwa kichapo kizito cha mabao 7-1 kutoka kwa Ujerumani ambao waliweza kutwaa ubingwa.

Je, mazingira kama hayo yanaweza kuwatoa kwenye reli Klopp na vijana wake? Wakati utazungumza katika hili.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*