Liver, Man City zazidi kunyukana ubingwa EPL

LONDON,England

TIMU za Liverpool na Manchester City zimeendelea kuchuana vikali katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England, baada ya jana kila moja kuondoka na ushindi  dhidi ya wapinzani wao.

Michezo hiyo iliyopigwa katika viwanja vya Selhurst Park na Anfield, Man City wakiwa ugenini waliweza kuondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Crystal Palace, huku Liver wakiwa nyumbani wakichomoza  kwa  ushindi wa mabao 2-0.

Katika mchezo ulioikutanisha Man City na Crystal Palace, alikuwa ni straika Raheem Sterling aliyewabeba mabingwa hao watetezi,  Manchester City kwa kuwafungia mabao mawili yaliyowafanya wapate ushindi huo wa  3-1  na kuwaweka kileleni mwa msimamo wa ligi kwa muda kabla ya Liver nao kupata ushindi wao huo  dhidi ya  Chelsea.

Man City  walipata bao lao la kuongoza dakika ya  15 wakati  Sterling alipoutumbukiza mpira wavuni na kisha akawahakikishia Man City pointi zote tatu akimalizia mpira wa krosi iliyopigwa na  Leroy Sane kipindi cha pili.

Sterling alipoteza nafasi ya wazi  dakika ya  10, baada ya kushindwa kumalizia pasi nzuri aliyotengewa na David Silva.

Hata hivyo straika huyo wa timu ya Taifa ya England muda mfupi baadae aliweza kufikisha bao lake la  20 kuifungia klabu yake  katika mashindano yote  aliyokwishacheza msimu huu akitumia pasi nzuri kutoka kwa Kevin De Bruyne na kisha akamchambua mlinda mlango wa Palace, Vicente Guaita.

Man City walipata bao la tatu kupitia kwa  Gabriel Jesus aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa tena na  De Bruyne, baada ya timu hiyo kufanya shambulizi la kushutukiza katika lango la wapinzani wao.

Bao la Palace lilipatikana dakika ya 81 ya mchezo huo kupitia kwa nyota wao,  Luka Milivojevic.

Wakati Man City wakifanya yao, Liver nao baadae wakafanya ya kwao kwa kuichapa Cheslsea mabao hayo 2-0

Kwa upande wao Liver, bao lao la  kwanza lilipatikana dakika ya 51 ya mtanange huo kupitia kwa nyota wao, Sadio Mane kwa kichwa akimalizia krosi iliyochongwa kutoka wingi ya kulia na Jordan Henderson kabla ya Mohamed Salah kupatichika la pili dakika ya 53 kwa shuti la mbali lililomshinda mlinda mlango, Kepa Arrizabalaga.

Dakika ya 59 na 61  Chelsea kidogo wapate bao, lakini mashuti yaliyopigwa na straika wao, Eden Hazard moja likagonga mwamba na la pili likaokolewa na mlinda mlango wa Liver, Alisson.

Kwa matokeo hayo Liver wamefikisha wamefikisha pointi 85 dhidi ya 83 za Man City ambayo hata hivyo ina mechi moja kibindoni.

 .     


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*