googleAds

Lampard alikubali kuwa nguruwe, asidai mabawa

NA AYOUB HINJO

KADRI siku zinavyosogea kupisha jua kuchomoza na kuzama kisha mwezi kuchukua nafasi yake kumulika anga wakati wa kiza kinene, kuna mambo mengi hutokea katika uso wa Dunia hii tunayoishi ndani yake.

Ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku ambayo yamekuwa hayaeleweki kwa baadhi ya watu, huku kwa wengine yakionekana kwenda sawa kama kupiga mstari mnyoofu na rula ya mita 30 tu.

Baada ya Harry Maguire na Aaron Wan-Bissaka, inawezekana jina la Frank Lampard likafuatia kutajwa mara nyingi zaidi duniani, sina takwimu maalum, lakini inaweza kuwa hivyo.

Katika michezo miwili tu, Lampard amekuwa maarufu zaidi ya mashuti yake makali aliyokuwa akipiga wakati huo akicheza soka.

Wapo waliobeti kwa kuweka fedha zao kwa kuamini atakuwa kocha wa kwanza kufukuzwa na kinyume chake. Wanasubiri kuona panga la Roman Abramovic likimpitia kama lilivyofyeka makocha waliopita bila huruma.

Manchester United na Liverpool ilikuwa michezo miwili iliyokuja haraka zaidi mbele ya Chelsea ya Lampard, ilikuwa mapema sana kwao kucheza dhidi ya vigogo hao.

Mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England walifungwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Old Trafford, ilikuwa stori kubwa kwenye vyombo vya habari duniani kote.

Kabla ya maumivu hayajapungua, wakalipoteza taji la UEFA Super Cup baada ya kukubali kichapo cha mikwaju ya penalti 5-4.

Kote huko Lampard alinyooshewa vidole, wapo wanaoamini alihitaji kujifunza zaidi kisha arudi Chelsea, lakini wengine wanaamini hakuwa mtu sahihi wa kupewa kazi hiyo baada ya Maurizio Sarri kuondoka.

Pamoja na hayo yote, kuna mambo mawili makubwa ambayo niliyaona katika michezo hiyo miwili ambayo Lampard alikiongoza kikosi cha Chelsea.

Hili linaweza kuwa jepesi zaidi, kikosi ambacho kimejaa majeruhi wengi, hasa wachezaji muhimu, huwa kinahitaji nguvu ya ziada kufanya vizuri.

Willian, Michy Batshuayi, Callum Hudson-Odoi, Ruben Loftus-Cheek na Antonio Rudiger ni sehemu ya wachezaji ambao hawajaonekana uwanjani mpaka sasa kutokana na sababu za majeraha.

Labda hata zile nne kutoka kwa Manchester United isingewezekana kufungwa kwa urahisi ule. Pengine stori ingekuwa tofauti.

Ni kwenye matatizo pekee ndipo mwanadamu hufahamu nguvu na uwezo ulio ndani yake.

Dhidi ya Liverpool, sura ya Chelsea ilibadilika, walikuja kivingine kabisa. Ilikuwa sapraizi kubwa kwa wapinzani wao, hawakuwa wepesi kama ilivyokuwa Old Trafford.

Ilikuwa Chelsea ambayo ilibeba matumaini kibao katika tabasamu la Lampard, wachezaji walipambana kwa ajili yake na timu, walikimbia kama mbwa kichaa aliyesaka chakula kwa ajili ya watoto wake.

Kipigo walichokipata kutoka kwa Manchester United kinaweza kuwa chanzo cha kuifufua timu hiyo au au kuizamisha, yote hayo yapo katika mabega ya Lampard.

Jambo kubwa linalowaumiza mashabiki wa Chelsea, ni aina gani ya msimu wanaenda kuwa nao? Kipi timu hiyo itafanya msimu huu? Na mambo mengine mengi.

Lampard amekutana na kitu tofauti ndani ya kikosi hicho, kivipi? Kwa takwimu za karibu zinaonyesha makocha waliopita walikutana na timu iliyokuwa na wachezaji wazuri kila idara, ilikuwa kazi kwao kuweka falsafa zao tu.

Chelsea ni moja ya timu ambazo wachezaji wake walidumu kwa zaidi ya miaka 10, lakini kikosi kile kinamomonyoka taratibu, wapo wachache ambao tayari wamechoka.

Kazi ya kwanza, Lampard anatakiwa kujenga kikosi hicho kukirudisha katika makali yake, ameanza kutoa nafasi kwa wachezaji kutoka akademi ya Chelsea, japo inaaminika imetokana na timu hiyo kufungiwa kusajili.

Lakini upande wa pili, swali la msingi inabidi liwe, Lampard anaweza kuwa kivutio kwa wachezaji wakubwa?

Historia yake ya kuvutia ipo katika upande wake mmoja tu, wakati akiwa mchezaji. Ukocha bado haujampa mafanikio, hata kama ingetokea angewapandisha daraja wale Derby County.

Kuondoka kwa David Luiz ni ishara tosha, wachezaji wakubwa wanafuata mafanikio. Mfano mwingine, unadhani dili la Paulo Dybala lisingefanikiwa kama Jose Mourinho angekuwa kocha wa Manchester United hadi leo hii?

Ole Gunnar Solskjaer hana tofauti na Lampard, bado hawana sura za kuvutia wachezaji wakubwa katika klabu zao, wanatakiwa kufanya kazi kubwa sana ili hilo liwe rahisi kama kutema mate chini.

Macho yote yapo kwa Lampard, kila mmoja anasubiri kuona kama atafanikiwa au atafeli, alichagua kuwa nguruwe, hana budi kutumia pua yake kufukua mihogo, kila kitu kinaonekana kuwa kigumu kwake, mabawa yatakuja baadaye.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*