KWIZERA AWACHANGANYA AKILI SIMBA

NA SAADA SALIM


 

SIMBA wameanza kuona umuhimu wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, raia wa Burundi Pierre Kwizera na sasa anaonekana kuwachanganya akili kutokana na kiwango cha hali ya juu  wanachoendelea kukionyesha akiwa  kwenye kikosi Rayon Sport cha nchini  Rwanda.

Simba waliachana na kiungo huyo katika msimu wa 2014/15 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,  kwa madai ya kushindwa kuonyesha kiwango, lakini  Julai, mwaka huu, Kwizera alitangazwa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda.

Kutokana na kiwango chake, Simba wameanza kujutia kuwa walifanya makosa kumtema kabla hajazoea mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na BINGWA jana,  mmoja wa viongozi wa Simba alisema  wameshtushwa na kiwango na Mrundi huyo, kwani amekuwa ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Rayon.

“Tunaendelea kufuatilia viwango vya wachezaji wetu walioondoka, kwa upande wa Kwizera tumeona kitu anachokifanya, kwa kweli tunavutiwa sana na uwezo wake na tunaamini tungeendelea kuwa naye angetusaidia,” alisema.

Akizungumza na BINGWA kwa simu kutoka Rwanda, Kwizera alisema anamshukuru Mungu, kwani anaendelea kufanya makubwa katika kikosi chake.

Kwizera alisema pamoja na kutemwa  bado ana mapenzi na Simba.

“Niseme tu kwamba, bado nina mkataba na Rayon Sport, mipango yangu ni kuzidi kupiga hatua mbele ila nawafuatilia sana Simba,  kwani ni timu ambayo niliichezea kwa moyo wangu,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*