KWANINI WAMBURA ANAJIONA ANAONEWA?

NA ONESMO KAPINGA

WIKI iliyopita Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Ebenezer Mshana, ilitupilia mbali rufaa  ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo, Michael Wambura.

Wambura alikata rufaa kupinga kufungiwa maisha kutojihusisha na masuala ya soka  na Kamati ya Maadili ya TFF, baada ya kubainika  kufanya makosa matatu.

Makosa yaliyomtia hatiani Wambura ni kupokea na kuchukua fedha za shirikisho za malipo ambayo hayakuwa halali, ikiwa ni kunyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013.

Kughushi barua ya kujieleza alipwe malipo ya Kampuni ya Jekc System Limited akijua  malipo hayo si halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili TFF Toleo la 2013.

Kosa jingine ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho ikiwa ni kinyume cha Ibara ya 50 (1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015).

Hayo yalikuwa ni mashtaka matatu yaliyowasilishwa na Sekratarieti ya TFF kwa Kamati ya Maadili ya TFF kabla ya kufungiwa maisha.

Baada ya kamati ya maadili kutoa uamuzi huo, Wambura aliita vyombo vya habari na kueleza hakupewa nafasi ya kujitetea, licha ya kumtuma wakili wake, Emmanuel Muga katika kikao cha kamati hiyo.

Katika mkutano wake  na vyombo vya habari, Wambura pamoja na kusema hakupewa nafasi ya kujitetea, lakini  alipinga  kufungiwa na kamati hiyo  kwa kuwa haikuwa na mamlaka.

Lakini mambo yote aliyoongea katika mkutano wake wa kwanza na nyombo vya habari, niliona kama anapiga porojo kwa kuwa aliacha kuzungumzia shtaka la msingi.

Nilitamani katika mkutano wake na vyombo vya habari angewathibitishia wanahabari kwa ushahidi usioacha shaka kuhusu mashtaka hayo aliyoshtakiwa nayo kwa kamati ya maadili, lakini badala ya kufanya hivyo alishusha tuhuma za matumizi mabaya ya fedha yalifayonyika kwa kipindi cha miezi saba na uongozi wa sasa wa TFF.

Nadhani hicho sicho ambacho  Watanzania walitaka kujua katika mkutano wake na vyombo vya habari, kwani wengi walitega sikio ili waweze kusikia kama alipokea na kuchukua fedha za TFF kinyume cha sheria.

Wambura hazungumzii kwa undani zaidi licha ya kusema suala hilo lilikuwa likichunguzwa na vyombo vingine vya dola.

Lakini suala la kujitetea katika chombo chochote kinachotenda haki si kwamba utetezi wa mshtakiwa unaweza kumfanya ashinde kesi, kwani wengi wanatoa ushahidi lakini mwisho anakutwa na hatia.

Wambura analijua hilo, lakini alionekana kutaka kuwaandaa Watanzania ili waone Kamati ya Maadili ya TFF inamwonea katika kutoa adhabu hiyo.

Najiuliza, kwanini Wambura ajione anaonewa wakati kuna watu wengine wamefungiwa kujihusisha na masuala ya soka na hawatumii vyombo vya habari kutaka kujisafisha?

Kama Wambura alishindwa kumweleza ukweli wakili wake kuhusu shtaka aliloshtakiwa na Sekretarieti ya TFF,  kwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo, unafikiri angeweza vipi kumtetea mteja wake?

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*