googleAds

KWA MK 14 HUYU, WATATESEKA SANA

LOVENESS BERNARD

ACHANA na kile alichokionyesha katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika kilele cha tamasha la klabu yake, yaani Simba Day, Meddie Kagere, ameendelea kuonyesha kuwa msimu ujao mashabiki wa timu pinzani watateseka sana.

Unajua ni kwanini? Si kwa ‘uchawi’ wala vinginevyo, bali ni kutokana na upambanaji wake awapo uwanjani kama alivyofanya dhidi ya Power Dynamos.

Katika mchezo ule uliochezwa Agosti 6, mwaka huu, Kagere alikuwa ni mchachakarikaji mno, akiwachachafya mabeki wa wapinzani wao hao unaweza kusema ilikuwa ni mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kumbe ni ya kirafiki tu.

Katika kuonyesha jinsi alivyopania kuendelea kula fedha za bilionea wa Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, mshambuliaji huyo amekuwa akifanya mazoezi ya hatari na wenzake hali inayowaacha hoi makocha wake na viongozi wengineo.

Katika mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, Kagere anaonekana kutotaka utani kabisa, kwani kila zoezi analopewa, hulifanya kwa ufanisi zaidi ya wenzake wote, tena akitumia nguvu na kila kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kama ni kukimbia, straika huwa hataki masikhara kama ilivyo katika mazoezi mengine, huku akionyesha madoido ya kila namna.

Mathalani, katika mazoezi ya juzi yaliyolenga kunoa safu ya ushambuliaji na ya ulinzi, Kagere alipangwa na Gadiel Michael ambaye alikiona cha moto kwani beki huyo wa kushoto alihenyeshwa barabara.

Pale palipohitajika nguvu, Kagere alitumia ubavu wake, lakini pia akili ilibodi na kumpa bonge la tizi Gadiel ambaye alijikuta akibaki kucheka tu asijue la kufanya wakati MK 14 huyo akichanja mbuga.

Ama kwa hakika, Kagere inaonyesha wazi kuna kitu amedhamiria kukifanya msimu ujao ambacho huenda kikawa somo kwa wachezaji wazawa ambao wamekuwa wavivu kupigania namba na kubaki kulalamika tu kuwa nyota wa kigeni wanapendelewa.

Juu ya Kagere, tayari Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amekiri kuwa anamtegemea mno nyota huyo wa kimataifa wa Rwanda.

Akizungumza na BINGWA hivi karibuni baada ya kutua nchini kutoka Afrika Kusini walikokuwa wameweka kambi, Aussems alisema: “Najisikia fahari kuwa na mchezaji kama huyu, anajitambua na anathamini heshima na nafasi aliyonayo Simba. Huyu namwona kama mtu muhimu mno katika kutimiza malengo yangu ya kuipa mafanikio Simba msimu ujao na mingine ijayo.

“Nikiwa na Kagere kikosini, huwa sina presha, nafahamu anaweza kufanya lolote muda wowote ule wa mchezo. Viongozi wa Simba (akiwamo Mo Dewji) na mashabiki, wanatakiwa kumwangalia Kagere kwa jicho la kipekee, hakika msimu ujao wataendelea kufurahi.”

Msimu uliopita, Kagere ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba kutokana na mabao yake yaliyoiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*