KWA MASTAA HAWA, GARI HALIJAWAKA EPL

LONDON, England


UHONDO wa Ligi Kuu ya England (EPL) umezidi kukoleza kasi yake, huku timu za Liverpool, Chelsea na Manchester City zikionekana kuuanza vizuri msimu huu, zikiwa hazijapoteza hata mechi moja kati ya nne zilizochezwa hadi sasa.

Hata hivyo, kama ilivyo kawaida ya EPL, matukio ya kushangaza huwa hayakosekani. Licha ya kwanza ni mwanzoni kabisa mwa msimu, tayari tumeshuhudia Man Utd wakitandikwa na Brighton (3-2) na Man City wakitoa sare na Wolves (1-1).

Lakini pia, iliwaacha wengi hoi kuishuhudia Tottenham ikitandikwa mabao 2-1 na Watford. Ni matokeo ya kushangaza kwa kweli na huo ndio utamu wa Ligi Kuu ya England.

Kwa upande mwingine, wapo mastaa waliokuwa wakitarajiwa kufanya vizuri msimu huu, lakini hadi kufikia raundi hii ya nne, mambo hayajakaa sawa kwa upande wao.

Leroy Sane (Man City)

Ukiacha ukweli kwamba hakwenda Urusi kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu, Sane alikuwa mchezaji muhimu wa Man City msimu uliopita, akikifungia kikosi hicho mabao 10 na kutoa ‘asisti’ 15.

Zaidi ya hapo, ndiye aliyeibuka mbabe katika vita ya kuiwania tuzo ya Kinda Bora wa EPL kwa msimu huo. Hivyo, matarajio ya wengi yalikuwa ni kumuona akiuwasha moto zaidi msimu huu, jambo ambalo halijatokea hadi sasa.

Mbaya kwake ni kwamba hajaingia ‘first eleven’ tangu kuanza kwa msimu huu na amepewa dakika 30 pekee katika mechi nne zilizopita na tayari kocha wake, Pep Guardiola, ameshasema Mjerumani huyo ameshuka kiwango.

Alvaro Morata  (Chelsea)

Licha ya msimu uliopita kuumaliza kwa tabu akisumbuliwa na majeraha, bado Morata aliweza kuipa Chelsea mabao 11 na kutoa asisti sita katika mechi za Ligi Kuu.

Msimu huu umeanza vibaya kwa upande wake, ingawa awali alitabiriwa kung’ara chini ya kocha mpya, Maurizio Sarri. Mhispania huyo amefunga bao moja pekee katika mechi nne.

Eric Bailly (Man United)

Hata katika mechi za ‘pre-season’ ungeweza kubaini udhaifu mkubwa wa eneo la beki wa kati katika kikosi cha Man United. Hata Jose Mourinho alihitaji mchezaji mpya katika nafasi hiyo, ingawa alifeli kumnasa.

Ukubwa wa tatizo ni kwamba katika mechi nne zilizochezwa, tayari Man United imesharuhusu mabao saba, huku Bailly, raia wa Ivory Coast akiwa sehemu ya ‘maboko’ yanayotokea.

Mechi pekee ambayo Man United waliondoka uwanjani wakiwa hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa ni dhidi ya Burnley, lakini hiyo ilikuwa ni baada ya Bailly kuingia uwanjani zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya kumalizika kwa mchezo.

Pierre Emerick Aubameyang (Arsenal)

Hakuna ubishi kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Gabon ni mmoja kati ya wachezaji muhimu Emirates. Lakini tangu kuanza kwa msimu huu hajaonesha kazi, huku bao pekee alilofunga likiwa ni dhidi ya Cardiff.

Lakini, bado mashabiki wa Arsenal wanaamini Mwafrika huyo atafufua makali yake ya kucheka na nyavu yaliyompa jina kubwa Bundesliga akiwa na Borussia Dortmund.

Andriy Yarmolenko (West Ham)

Usajili wake uliwafanya mashabiki wa West Ham wakae mkao wa kula kusubiri makali yake dhidi ya mabeki wa timu nyingine. Yarmolenko alikuwa kwenye ubora wa juu akiwa na Dynamo Kyiv, ambapo aliondoka akiwa ameifungia mabao 137.

Hata hivyo, nyota huyo aliyesajiliwa na kocha mpya, Manuel Pellegrini, hajaonesha lolote hadi sasa. Mbaya zaidi ni kwamba katika mechi nne, West Ham imepoteza zote na sasa inaburuza mkia.

Fred (Man United)

Huenda ni changamoto ya kukabiliana na ligi mpya, lakini ukweli ni kwamba bado Fred hajaonesha kilichoivutia Man United akiwa na Shakhtar Donetsk ya Ligi Kuu ya Ukraine.

Fred, ambaye msimu uliopita alijizolea umaarufu mkubwa barani Ulaya kwa pasi zake, aliishia benchi wakati Man United ikimenyana na Burnley hivi karibuni.

Ryan Sessegnon (Fulham)

Misimu kadhaa iliyopita, alitabiriwa kufikia ‘levo’ za staa Gareth Bale au Marcelo na ni kutokana na kazi zake zilizoiwezesha Fulham kurejea Ligi Kuu ya England. Aliipandisha daraja akiwa amefunga mabao 16 na kutoa asisti nane.

Msimu huu, Sessegnon mwenye umri wa miaka 18, ameingia kikosi cha kwanza mara mbili pekee na mbaya wake ni Andre Schurrle, anayepewa nafasi kubwa ya kucheza winga.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*