KUTOJIAMINI KUNAVYOCHANGIA USALITI

NA RAMADHANI MASENGA


TUNAPOZUNGUMZIA chanzo cha usaliti tunazungumzia uwanja mpana mno, japo akili na fikra za watu wengi huwa hazipendi kufanya hivyo na huamini suala moja tu kwamba msaliti ni malaya mpenda ngono au pesa.

Wengi huwa hawapendi kuangalia vyanzo vya usaliti wenyewe na kutokana na tabia hii, ndiyo maana usaliti bado unaonekana ni tatizo lisilo na mwarobaini. Yote ni kutokana na wengi kuangalia sababu moja tu, tena kwa vigezo dhaifu.

Kushindwa kutibu chanzo ambacho kimsingi ndicho kiini cha tatizo, imepelekea usaliti kuendelea kuonekana kama suala gumu kuepukika.

Ni vyema tukawekana wazi, wengi wanaotenda usaliti huwa na sababu. Ndiyo, huwa na sababu hata kama sababu zenyewe zitaonekana kama si za maana bali kwao huwa na maana.

Kwa mfano wapo baadhi wanaosukumwa kufanya usaliti huwa na kitu hiki. Kutojiamini. Yes, kutojiamini!

Kwa kiasi kikubwa hali hii imesababisha wengi kufanya usaliti bila wengi ama pengine hata wao wenyewe kujua kama hili ni tatizo. Tatizo lenyewe huanzia hapa.

Mtu asiyejiamini huwa na wasiwasi karibu kwa kila kitendo cha mwenzake. Akiambiwa anapendwa atafurahi kwa dakika moja kisha inayofuata atawaza kama alichoambiwa ni kweli au anadanganywa.

Kutokana na hali hiyo huanza sasa kuwa na umakini uliokithiri katika matendo ya mwenzake, ili apate kujua kama kweli anapendwa kama kauli ya mwenzake ilivyo.

Mara nyingi katika hili hujikuta wakipata wasiwasi zaidi. Maana katika hali ya kawaida huenda akamwona mwenzake akiongea na mwanamke/mwanaume sehemu, kutokana na hali yake atawaza tofauti. Hata namna ya kumuuliza pia huwa tofauti.

 Hawezi kumuuliza taratibu au kawaida ni lazima tu hali fulani isiyo ya kawaida ijitokeze. Sasa hapa huwa kuna tatizo lingine.

Mkisiwa yaani mpenzi wa yule asiyejiamini wakati mwingine huwa anaghadhibika kutokana na kuhisiwa kuwa na mahusiano na mtu mwingine kitu ambacho huwa si kweli.

Katika hali hiyo na yeye hujikuta akitoa majibu kwa hasira kuoneshwa ni kwa kiwango gani anakereka kwa anavyosingiziwa. Hapo hali huwa inazidi kuwa mbaya. Kwa sababu  baada ya kujibiwa kwa ukali na hasira huchukulia hasira hizo kama dharau na kuanza kuamini kuwa mwenzake anajihusisha na mtu mwingine.

Hapo ataanza kuvuta picha karibu kwa kila kosa la kimaongezi mwenzake aliyowahi kufanya. Iwe labda kuna siku alitoa sentesi ambayo hakuielewa au kuna hali ya kutofautiana iliwahi kuzuka baina yao. Pia huwa haishii hapo tu.

Huanza pia kuangalia baadhi ya vitu ambavyo hakubarikiwa navyo. Kama vile mwonekano mzuri, pesa au kuwa na mavazi ya gharama.

Akimaliza hapo huanza kuchanganya picha na aina ya watu ambao amewahi kukuona ukiongea nao. Akimpata hata mmoja kati yao kuwa kuna kitu kamzidi, basi hapo huanza kuwa na imani na hisia zake. Moja kwa moja huanza kujiridhisha kuwa hakukosea pale mwanzo alipokuwa na hisia kuwa mwenzake ni msaliti.

Asiyejiamini huwa haishiwi sababu za kumfanya kuamini anasalitiwa. Hata kama ana pesa, mwonekano mzuri au hata pengine ni mtu maarufu mahala alipo, ubongo wake haushindwi kutengeneza sababu nyingine.

Kwa mfano anaweza kuanza kuhisi labda hamfurahishi mwenzake faragha, hivyo mwenzake anaweza kumsaliti kwa sababu hiyo. Maisha haya ya wasiwasi na hofu huwa hata wenyewe hawafurahishwi hayo. Mara nyingi huwa wanatumia mbinu hii.

Ili kujiweka katika mazingira ambayo wao huona yanaweza kuwapunguzia hali ya sononeko katika nafsi na wao hujikuta wakizama katika mtego huu. Usaliti.

Huona wakiwa na mahusiano na watu wengine katika namna flani inaweza angalau kuwapa ahueni katika nafsi zao kutokana na mashaka waliyonayo. Miongoni mwa watu wenye tabia ya kutojiamini imekuwa kawaida kwao hali hii.

Wameamua kuwa na mahusiano na watu wengine ili kujipa faraja na nafuu ya nafsi zao. Wamefanya hivi wakiamini kwa nia njema kabisa. Wakiamini ni kuweza kupata faraja na ahueni ya maisha yao. Kitu ambacho mara nyingi pia huwa hakitokei.

Asiyejiamini siku zote huwa haishiwi na wasiwasi. Hata akiwa na mahusiano ya watu wangapi. Ila wao mara nyingi huwa hawalitazami hili, ndiyo maana kila siku bado utakuta wakiwapanga wengine misururu katika orodha ya wapenzi wao.

Kwa maana hata baada ya kuwa na mwingine kufuatia kuona mpenzi wake wa mwanzo anampa wasiwasi huona na huyu mwingine kama yule pia. Tabia yake ya kutafsiri kauli na mambo tofauti huwa bado hajaiacha wakati ndiyo mzizi wa hangaiko lake katika nafsi. Wengi wa watu wa namna hii kila siku huona mapenzi kama mchezo wa kuigiza kutokana na mtazamo hasi kwa kila tendo kutoka kwa mwenzake.

Kwa mtu wa aina hii kama hajapata msaada wa  ushauri wa kitaalamu si ajabu kumwona kila siku akiachwa na wapenzi wake kwa sababu ya usaliti, huku yeye akiamini alifanya hivyo kwa nia njema. Tatizo hili huwasumbua wengi hasa vijana.

Leo ukikuta maongezi katika maskani ya vijana wengi inayozungumzia mapenzi wengi, wanajisifu kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja. Kila mmoja atajifaharisha kwa kuwa  mahiri wa kumiliki wapenzi wengi. Ila wote ukiwachunguza kwa makini utajua kuna kitu wanakosa. Wote wanakosa ile hali ya kufurahia mapenzi. Huwa wanafurahia ngono tu.

Na siyo kuwa wanatamani kuwa katika hali hii siku zote. Hapana. Ila ni kwa kuwa hawajajua namna ya kujitoa katika  mfumo huo wa maisha na kubaki salama bila kuwa na wasiwasi na wenza wao. Mwenza wako yupo namna hii?

Kila tendo ukimwambia kama haamini hivi! Kila ukimuaga  unaondoka anahisi unyonge unyonge hivi. Yuko hivyo mpenzi wako?

Kaa na zungumza naye namna unavyompenda na kumjali na kiwango gani ana thamani katika maisha yako. Achana na tabia zote unazohisi zinasababisha kuleta utata katika akili yake. Mara nyingi penda kumsikiliza na kumjibu kwa sauti ya upole na iliyojaa mapenzi. Tofauti na hapo kuna wasiwasi wa kumpoteza kipenzi chako.

Kutojiamini ni tatizo na wakati mwingine tunaweza kuita ni ugonjwa. Jitahidi kumsaidia kadiri utakavyoweza  ili aweze kuepukana na suala hili. Ni suala lenye athari kwake, kwako na katika maisha yenu kijumla. Si  kila msaliti   huwa anapenda. Hapana! Sababu ziko nyingi  na hii pia huwa miongoni.

Kuiacha tabia hii kwa mpenzi wako ni sawa na kuruhusu mahusiano yako baadaye yapate shida na karaha. Onesha kumjali na kujali mahusiano yako kwa kumsaidia kuondokana na tabia hii badala ya kumwacha kuendelea nayo.

Inaposemwa wapenzi ni muhimu kusaidiana isiwe katika vipato tu, hata katika masuala kama haya pia msaada ni muhimu. Ubora wa mpenzi wako ni ubora wa mahusiano yenu. Na ubora wa mahusiano yenu ni furaha katika maisha yenu.

Katika hali yoyote jitahidi kumfanya kuwa bora zaidi ili uweze kuwa katika mahusiano ya raha na amani. Kumwacha aangamie katika hali hiyo ni kuyaacha mapenzi yenu yafuate njia ambayo si sahihi na mwisho wa yote ni kutengana ilhali mkiwa bado mnapendana.

Instagram:ramadhan.masenga

ramadhanimasenga@yahoo.com


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*