KUMBE RUBANI ALIJUA AJALI YA WACHEZAJI WA CHAPECOENSE

MEDELLIN, Colombia

Abiria 76 wakiwamo wachezaji wa klabu ya Chapecoense wamefariki dunia kwa ajali ya ndege nchini Colombia, baada ya kulazimishwa kupanda ndege hiyo yenye hitilafu.

Rubani Mick Quiroga ambaye anachukuliwa kama shujaa, aliuliza kama wachezaji hao wa klabu ya Brazil, Chapecoense ambao walikuwa wanakwenda kwenye mchezo wa fainali kama wangeweza kupelekwa moja kwa moja mjini Medellin badala ya kupitia nchini Bolivia.

Lakini mamlaka ya anga ilikataa ruhusa ya timu hiyo kupelekwa moja kwa moja kutoka mjini Sao Paulo nchini Brazil hadi Medellin, Columbia.

Chombo cha kurekodia sauti kimenasa mazungumzo ya rubani huyo wa Shirika la Ndege la Bolivia la LAMIA, jinsi alivyokuwa akimbembeleza meya wa mjini Chapeco itapotokea timu hiyo ya Chapecoense, akiomba msaada ili apewe ruhusa ya kwenda moja kwa moja hadi mjini Medellin.

Lakini meya huyo alikataa, akisema: “Nimekodisha ndege ya Bolivian ibebe timu kutoka mjini Sao Paulo hadi Santa Cruz. Nitakuwa nawasubiri hapo Santa Cruz.

Pamoja na rubani kujitahidi kuomba lakini Wakala wa Taifa wa Usafiri wa Anga nchini Brazil (ANAC) walikataa kutokana na sheria za usafiri wa anga za nchi hizo ambazo zinasema maamuzi ya kubadili safari yanapaswa kufanywa na mamlaka za anga ya Brazilian au Colombia.

Baada ya wachezaji hao kulipia ndege hiyo ya LAMIA kutoka Brazil, walipaswa kwenda hadi nchini Bolivia, ambapo walitua Jumatatu usiku, huenda wachezaji na abiria wengine wangeepuka ajali hiyo kama ombi la rubani la kwenda kutua moja kwa moja mjini Medellin lingekubaliwa.

‘Micky’ Quiroga alifariki dunia pamoja na abiria 75 wakati ndege hiyo iliyotengenezwa nchini Uingereza kuanguka kwenye milima jirani na Mji wa La Ceja.

Amesifiwa kwa ushujaa wake baada ya kumwaga mafuta kutoka kwenye ndege hiyo muda mfupi kabla ya kuanguka ili kuepusha ndege hiyo kuungua.

Ingawa bado uchunguzi unafanyika kujua chanzo cha ajali hiyo, lakini kuna hofu kwamba tatizo lilikuwa ni la umeme.

Pia kuna mtaalamu ambaye atasaidiana na mamlaka za ndege za Uingereza, ambaye amedai kwamba ndege hiyo iliisha mafuta dakika tano kabla ya kutua ilipotarajiwa katika Uwanja wa Ndege wa Jose Maria Cordova nje ya Mji wa Medellin.

Msemaji wa Wakala wa Anga wa Taifa nchini Bolivia, amesema ndege hiyo ilichunguzwa kabla ya kuondoka Colombia na haikuwa na tatizo lolote.

Mamlaka za anga zilipata tabu sana kuwaokoa watu sita waliookoka katika ajali hiyo iliyopoteza uhai wa watu 76, ikiwa ni janga kubwa kutokea kwa mwaka huu.

Timu hiyo ya Ligi Daraja la Kwanza ambayo kocha wake, Caio Junior, amekuwa akiita ‘Leicester City ya Brazil’, ilikuwa ikielekea kwenye fainali ya Copa Sudamericana nchini Colombia, mechi ambayo ilikuwa ya kihistoria kwao.

Timu hiyo ambayo ilibakisha dakika tano kabla ya safari yao kumalizika, walikuwa wakienda kucheza mchezo huo wa kwanza wa fainaili dhidi ya Atletico Nacional, ambapo mechi hiyo ilitarajiwa kupigwa leo alfajiri katika Uwanja wa Atanasio Girardot mjini Medellin.

Taarifa kutoka kwenye redio moja nchini Colombia, ilisema kwamba timu hiyo ilikodishiwa hoteli ya nyota tano iitwayo San Fernando, hoteli kubwa mjini Medellin.

Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL) wamesimamisha mashindano hayo.

Mazingira yasiyo rafiki yalisababisha gari za wagonjwa kushindwa kufika kabisa kwenye eneo la tukio, ambapo wafanyakazi wa gari ya wagonjwa walisema kwamba walipaswa kubeba walionusurika na ajali hiyo mwendo wa dakika 30 kutoka eneo la tukio na kuwapeleka hospitali kutokana na ajali hiyo kutokea eneo la milima.

Baada ya kutembea umbali huo wa miguu, walikuwa wakiwapakiza kwenye malori ambayo yalitembea mwendo wa kilometa 700 hadi kufikia magari ya wagonjwa yalipoegeshwa, lakini kuna wakati malori hayo yalikwama kwenye matope na kufanya kazi hiyo ya kuwasaidia majeruhi kuwa ngumu.

Tatizo jingine lililowasumbua katika kutoa huduma ya kwanza lilikuwa ni joto la mwili, ambapo walikuwa na kazi ngumu ya kuwasaidia walionusurika kutokana na eneo hilo kuwa na baridi kali ya sentigredi tano.

Alan Ruschel, beki anayecheza kwa mkopo timu hiyo ya Chapecoense akitokea klabu ya Internacional, alikuwa mchezaji wa kwanza kutajwa kuwa ni mmoja wa wachezaji walionusurika na ajali hiyo.

Mchezaji mwingine Jakson Follmann, mwandishi Rafael Hansel, mhudumu wa ndege Ximena Suarez na fundi Erwin Timiri pia walinusurika katika ajali hiyo.

Mtangazaji wa Fox Sports nchini Brazil, Paulo Julio Clement naye alinusurika katika ajali hiyo mbaya iliyouwa waandishi 21.

Taarifa kutoka Catalonia zinasema mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi na wachezaji wenzake wa Argentina, walitumia ndege hiyo iliyopata ajali mjini Medellin, walipokuwa wakisafiri kwenda kucheza na Brazil, mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 mjini Belo Horizonte na kufungwa mabao 3-0.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*