KUMBE HATA FERGUSON ANAIOGOA MADRID

MADRID, Hispania

KIKOSI cha sasa cha Real Madrid kimeonekana kumtisha kocha wa zamani wa Manchester United, ambapo amesema haitakuwa rahisi kwa timu nyingine kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika michuano ya mwaka huu, Madrid wamepangwa na Kundi H wakiwa na Borussia Dortmund, Tottenham na APOEL.

Ferguson alisema ni kweli Juventus wako sawa kwa sasa, lakini kuivua Madrid taji la michuano hiyo itabaki kuwa stori.

Msimu uliopita, Madrid waliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kubeba mara mbili mfululizo taji hilo, baada ya kuwachapa Juve mabao 4-1, katika mchezo wa fainali.

Mkongwe huyo raia wa Scotland alidai kwamba haoni sababu ya kocha Zinedine Zidane kukosa ubingwa wake wa 13.

“Nafikiri Juventus wanatawala ligi ya Italia. Wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka sita iliyopita. Wana kocha mzuri,” alisema Ferguson.

“Unatakiwa kuelewa jinsi Real Madrid walivyo wazuri kwa sasa. Ni timu iliyokomaa, wamekuwa pamoja kwa miaka mitatu, minne, na mitano.”

Juve wako Kundi D, ambapo watachuana na Barcelona, Sporting Lisbon na Olympiacos katika kuisaka nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora.

Aidha, Ferguson aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, anaisikitikia Liverpool katika harakati zake za kumzuia kiungo wake, Philippe Coutinho.

Kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili jana, Coutinho alikuwa akifukuziwa kwa udi na uvumba na mabosi wa Barca, ambao waliweka mezani kiasi cha Pauni milioni 199.

Liver walitajwa kuzitolea nje ofa tatu za Barca, wakisistiza kuwa, Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 25 ana umuhimu mkubwa kikosini, hivyo hawako tayari kumpiga bei kwa kiasi chochote cha fedha.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*