googleAds

KOTEI AOMBA RADHI YANGA

NA ZAITUNI KIBWANA

Siku  moja baada ya uongozi wa Yanga kupiga hodi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), beki wa Simba, James Kotei, ameibuka na kuomba radhi kwa mashabiki wa timu hiyo kwa kitendo chake cha kumpiga beki wao, Gadiel Michael.

Kotei alionekana kwenye vipande vya picha vya mechi ya Watani wa Jadi akimpiga Gadiel, huku mwamuzi Jonesia Rukyaa akiwa hajaona tukio hilo kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya 0-0.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Kotei alimuomba radhi Michael kwa kitendo chake alichofanya kwenye mchezo huo.

“Wapendwa wanasoka, mpira ni mchezo wa amani na si vita kama wengi wanavyodhani, itabaki kuwa hivyo milele, ikiwa ushindani ulitufanya kuvuka mipaka lakini hicho si kisingizio cha kufanya kutokuwa waungwana, baada ya kusema hayo nachukua nafasi hii kuomba radhi kwa rafiki na mchezaji mwenzangu Michael kwa yaliyotokea kwenye derby, naungana na wadau wa soka kwa wanaokemea kitendo kile, sisi ni familia moja, iwe Simba au Yanga, na mpira ni baba yetu na hili halitajitokeza tena,” aliandika Kotei kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kwa upande wake Gadiel, naye aliguswa na andiko la msamaha la Kotei, naye akaandika kujibu ujumbe ule:

“Uungwana ni vitendo siku zote, nimepokea kwa mikono miwili msamaha wa Kotei kwa kitendo alichonifanyia, bado tutabaki kuwa familia moja ya mpira na pia nitaendelea kukuheshimu kama kaka yangu,” aliandika Gadiel.

Kauli hiyo ya Kotei imewafurahisha viongozi wa Yanga, ambapo Msemaji wake, Dismas Ten, alimsifu kwa kitendo hicho cha kiungwana.

“Nilisema jana, Kotei ni mchezaji muungwana na hana rekodi za matukio ya kihuni uwanjani kwa mujibu wa kumbukumbu zangu, hongera kwa kutambua kosa lako,” alisema Ten.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*