KOSA LA KIJINGA WANALOFANYA WANAWAKE SIKU ZOTE

NA RAMADHANI MASENGA

KUPENDANA ni suala linaloweza kuja lenyewe tu. Ila kudumu katika uhusiano si suala linaloweza kujileta lenyewe. Hapa inahitaji ujanja, umakini na umahiri.

Sababu ya mahusiano mengi kuishia njiani japo wahusika walipendana na kuheshimiana, ni hali ya kukosa umakini, ujanja na umahiri.

Kwa mfano, wanawake wengi wanapoteza mvuto kwa wanaume katika siku za kwanza za mahusiano yao kwa sababu ya tabia ya wengi wao kupenda kutangaza shida mapema. Iko hivi.

Hata mwanamume awe na hali njema kwa kiwango gani, ila huwa na wasiwasi sana pale anapoona mwanamke anayempenda anatanguliza sana shida zake za kifedha katika siku za mwanzo za kujuana kwao.

Ili mwanamume ajiaminishe kwamba yuko na mwanamke sahihi, ni jukumu la huyo mwanamke kuthibitisha hivyo. Katika kuthibitisha huko, mwanamke husika kwa namna yoyote anatakiwa kwanza kuzungumzia mambo mengine ya kujenga, kufurahisha hata ya kutaniana ila si suala la fedha mapema.

Wanaume wengi huwaona wanawake wenye kupenda kuomba pesa katika siku za mwanzo za kujuana kwao kama watu wasiojielewa na wenye tamaa. Mtu asiyejielewa na mwenye tamaa ni malaya kwa tafsiri ya wanaume wengi.

Unakuta mwanamke amejuana na mwanamume wiki moja tu ila ataanza kuomba pesa ya kusuka, ya kununua simu mpya ama hata ya kodi ya nyumba. Zamani dada kwani ulikuwa unaishi vipi? Ama kila mwanamume uliyekuwa ukikutana naye ulikuwa unamuomba pesa?

Mwanamume anaweza kumpenda sana mwanamke. Anaweza kuwa na mipango naye mingi sana. Ila kama mwanamke huyu atatanguliza mapema shida zake, ajue hawezi kudumu na mwanamume huyu.

Wanaume kujisogeza kwa wanawake haimaanishi wamekusanya fedha sasa wanataka watu wakutumia nao. Hapana. Mwanamume mwenye nia ya kuanzisha mahusiano makini, hujisogeza kwa mwanamke kwa ajili ya kumpima kama anastahili kuwa naye katika maisha.

Sasa mwanamke akibabaika na kuanza kuomba uomba hela katika siku za mwanzo za kujauana kwako, mwanamume husika ataona kipimo chake kimeonesha virusi vya tamaa na ujinga kwa mwanamke huyo. Hivyo taratibu atajiweka mbali.

Wanawake wengi wanalalamika kwamba wanakuwa na wanaume miezi kadhaa kisha wanaume hao wanakimbia. Ndiyo, lazima wakimbie. Asikimbie kwanini kila siku unamfanya kuwa ATM? Asikimbie kwanini kila siku wewe tu ndio unaleta shida zako mezani?

Mwanamke makini hata akiwa na shida huwa hazioneshi katika siku za mwanzo za kujuana na mwanamume husika. Katika siku za mwanzo, mwanamke huyu atajitahidi kadiri awezavyo kuficha shida zake ila atajiweka katika nafasi ya kuonesha anamsikiliza zaidi mwanamume wake.

Katika namna hii, mwanamume huyu anajikuta akimuona mwanamke huyu ni sahihi. Hata mwanamume huyu akimwambia mwanamke wake kwamba amepata fedha nyingi katika biashara ama kazi zake, mwanamke makini atamshauri namna bora ya kutumia pesa zake.

Mwanamke huyu hafanyi hivi kwa sababu hana shida ya fedha ama mjinga. Hapana. Anafanya hivi ili aweze kuaminika na aweze kutafsirika vizuri na mwanamume huyu.

Mwanamume akishamwamini mwanamke husika, akamuona kwamba ndiye mtu sahihi wa kuishi naye, hawezi kuona udhia hata mara moja katika kumtatulia shida zake. Atajiuliza, kama nikiacha kumtatulia shida zake mimi nani mwingine amtatulie?

Na huyo mwingine akimtatulia, mwanamke huyu makini kama alivyo ataendelea kuwa na mimi? Kwa woga wa kumpoteza mwanamke huyu ambaye akili yake tayari inakuwa imemtafsiri kama mwanamke sahihi, anajikuta akimpatia kila anachotaka.

Njia ya kupata mahitaji kwa mwanamume si kumuombaomba pesa. Kwanza ni kuonesha kutoihitaji sana fedha yake huku ukijikita zaidi katika kuonesha kuguswa zaidi na matatizo yake kuliko kuongelea matatizo yako.

Wanaume wengi makini wanatafuta wanawake wa kuwafariji na kuwatia nguvu. Wanatafuta wanawake wenye kuonesha kuwahitaji zaidi wao kuliko fedha zao.

Ukionesha shida za fedha mwanzoni wa mahusiano yenu, si tu mwanamume husika ataona yuko kwa mtu ambaye si sahihi ila pia atajiona alichofikiria mwanzo sicho.

Wanaume wenye nia madhubuti ya kuishi na wanawake, huwa  wanaumizwa sana na wanawake wapenda kuomba pesa. Yote hii ni kwa sababu wanahisi wameingia katika mikono ya wanawake wanaowafanya wao mabuzi.

Shida ya mwanamke inatekelezwa na mwanamume baada ya mwanamke husika kufanikiwa kuteka akili na hisia za mwanamume.

Na haiwezekani kuwa umefanikiwa kuteka hisia na akili zake katika siku za mwanzo za kujuana kwenu. Ni kweli, mwenzako anaweza kuonesha kakamatika sana katika siku za mwanzo tu toka mjuane.

Ila hiyo isukupe imani kwamba tayari umemteka kisawasawa na hivyo uanze kulia shida zako. Hapana.

Hata kama anaonesha kukupenda ila katika siku za mwanzo ukiwa omba omba, utamfanya ajitafakari sana kama sehemu anayojiachia ni sehemu salama kwake.

Wanawake wengi wameachwa kwa sababu ya kuendekeza shida. Yaani kila siku wao shida, kila meseji anayomwandikia mpenzi wake ndani yake kashaomba hela. Hata kama mwanamume huyu anampenda huyu mwanamke ni lazima tu akimbie.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia (Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*