googleAds

KOCHA SIMBA ATAOGA NOTI ZA MO

NA ZAINAB IDDY

SVEN Ludwig Vandenbroeck ataoga noti za Mohammed Dewji ‘Mo’, iwapo ataendelea na kasi aliyoanza nayo jana alipotua kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Bunju (Mo Simba Arena), jijini Dar es Salaam.

Ikiwa ni siku moja baada ya kutangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Simba kuchukua mikoba ya Patrick Aussems aliyetimuliwa, Vandenbroeck hakutaka kulaza damu na badala yake, alianza kufanya kile kilichomleta Tanzania.

Ukiachana na kuwasili kwake mazoezini jana, kuna matukio matatu yaliyofanywa na kocha huyo kumwonyesha ni wa aina gani na kuthibitisha kauli ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza kuwa wamepata mtu wa kazi hasa.

Tofauti na ilivyo kwa makocha wengi siku zao za kwanza mazoezini, Vandenbroeck hakutaka kulemba na badala yake aliingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kuteta mawili matatu na meneja wa timu, Patrick Rweyemamu.

Baada ya hapo, alitoka na kuchukua kiti kukaa pembeni mwa uwanja akiwa na kitabu chake kidogo na kuanza kufuatilia mazoezi ya timu yake hatua kwa hatua na kumsoma mchezaji mmoja mmoja.

Kila mchezaji alipofanya kitu adimu kama kupiga pasi ya maana, kutoa pasi ya bao, kufunga au kumiliki mpira kwa aina ya kipekee, aliandika katika kitabu chake hicho huku akiwa makini mno (serious).

Kati ya wachezaji ambao wameonekana wazi kuingia katika kitabu chake hicho jana ni Ibrahim Ajib ambaye alifunga bao, lakini pia kuonyesha mbwembwe zake za kumiliki mpira na Meddie Kagere ambaye alicheka na nyavu mara tatu.  

Wengine ni Francis Kahata aliyefunga bao moja, Sharaf Shiboub na Pascal Wawa ambao wote walitoa mapande ya mabao (assist) kwa Kagere.

Na baada ya mazoezi, kocha huyo alizungumza na wachezaji kabla ya kuwapa mkono mmoja baada ya mwingine.

Kwa kifupi, Vandenbroeck anaonekana wazi kuwa mtu makini na asiye na mbwembwe zaidi ya kuzingatia kazi yake akifahamu hilo ndilo hasa wanalolitaka Simba na mwekezaji wao, Mo Dewji, lakini pia bosi Mazingiza.

Ni wazi iwapo Vandenbroeck ataendelea na kasi yake aliyoanza nayo jana na kuipa mafanikio makubwa Simba, atakula fedha za Mo na Wanamsimbazi kwa ujumla mpaka ‘azikinai’.

Ikumbukwe kati ya mambo yaliyochangia kumwondoa Aussems Simba ni kutokuw amakini na kazi yake, akishindwa kuheshimu maelekezo ya mabosi wake na klabu wka ujumla.

Vandenbroeck aliwasili kwenye uwanja huo wa Simba saa 9:45 akiwa katika gari namba T 927 DQB, aina ya Wsth, akiongozana na kocha wa viungo, Adel Zrane.

Baada ya kufika alitumia dakika tano kuwa ndani ya gari hiyo kabla ya kushuka na kwenda moja kwa moja katika vyumba vya kubadilishi nguo wachezaji, akiongozwa na Rweyemamu.

Baada ya dakika tano, alitoka na kukaa katika kitu na kuangakia mazoezi yaliyokuwa yakisimamiwa na kocha msaidizi, Seleman Matola na kuanza rasmi majukumu yake kwa kumsoma mchezaji mmoja mmoja.

Katika hatua nyingine, Vandenbroeck alishangazwa na mashabiki wengi wa Simba waliojitokeza uwanjani hapo ambao walianza kumshangilia huku wakipiga makofi na miruzi hivyo naye kulazimika kuwapungia mikono

Katika mazoezi hayo, Zrane aliwakimbiza wachezaji kwa kuzunguka uwanja mara sita sawa na meta 10050 kwa lengo la kutafuta pumzi na baadaye kunyoosha viungo kabla ya ‘kumpasia mpira’ Matola.

Mtihani kwa kwanza mkubwa wa Vandenbroeck utakuwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga utakaopigwa Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*